TPDC Limewezesha Uchumi wa Viwanda

Mhandisi wa Uendeshaji wa Bomba la Gesi, Ndugu Hassan Temba akiwaeleza kwa vietendo Wahairi wa Habari namna ambavyo wanaendesha na kusimamia bomba la gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam kwa urahisi zaidi wakiwa kwenye Chumba cha Uendashaji na Usimamizi wa Gesi Asilia Kinyerezi kwa msaada wa vifaa maalum vya mawasiliano vilivyowekwa kwenye mundombinu ya gesi asilia.

“Kukamilika kwa Miundombinu ya Taifa ya kuchakata na  kusafirisha gesi asilia pamoja utafiti wa kina wa gesi asilia uliofanyika na kupelekea kugundua kiasi cha gesi asilia cha futi za ujazo trilioni 57.55 pamoja na utafiti unaondelea kufanyika katika baadhi ya maeneo nchini yakiwemo ya Ruvu na Eyasi Wemberi ni sehemu ya mikakati kabambe ya TPDC katika kuiwezesha Tanzania kujenga uchumi imara na endelevu wa viwanda”

Haya yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Utawala TPDC, Ndugu Hans Mwambuba ambaye alimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wakati akifungua warsha ya siku moja kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyobeba mada kuu ya Mkakati wa TPDC kuelekea Tanzania ya Viwanda iliyoifanyika katika Kituo cha Kupokelea Gesi Asilia cha Kinyerezi mwishoni mwa wiki.

Ndugu Hans amewashukuru kwanza wahariri kwa kutoa muda wao na kukubali wito wa kuhudhuria warsha hiyo ya siku moja na kwamba ni matumaini yake na ya shirika kuwa kiu ya kutaka kufahamu kiundani mikakati ya TPDC kuelekea uchumi wa viwanda ndio iliyowafanya wahudhurie semina hiyo kwa lengo la kujijengea uelewa mpana na sahihi wa TPDC na shughuli zake ili waweze kupelekea taarifa sahihi kwa wananchi.

Akiwa anamkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Meneja Mawasiliano wa Shirika hilo ambaye Kitengo chake ndicho kimeandaa na kuratibu Warsha hiyo ameeleza kuwa “Sisi kama Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania tunatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha na kuuhabarisha umma na ndio maana tumekuwa tunafanya warsha kwa wanahabari nchi nzima na leo hii tunayofuraha kuwa nanyi wahariri katika warsha hii yenye lengo kubwa la kuwaongezea ufahamu sahihi wa sekta ya mafuta na shughuli za TPDC na makampuni yake tanzu ya GASCO na TANOIL ili muweze kutoa taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu shughuli za shirika lakini pia sekta ya mafuta kwa ujumla wake”

Akielezea mikakati ya TPDC kuelekea Uchumi wa Viwanda ndugu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ameeleza kuwa “Matumaini ya kujenga uchumi bora wa viwanda nchini tuliweza kuyaleta mara baada ya kukamilika kwa mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo Songo Songo mkoani Lindi na Madimba mkoani Mtwara pamoja na bomba kubwa la kusafirishia gesi hiyo hadi Dar es Salaam na kikubwa kwenye miundombinu hii ni kwamba imefungua fursa ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa yote iliyopita na hii ni kwasababu muwekezaji ana uwezo wa kuunganishiwa gesi asilia kama nishati ya kuendesha mitambo au kuzalisha umeme wa kutumia kwenye viwanda”

Ameongezea kuwa kutokana na bomba hilo tayari tumeunganisha gesi kwenye kiwanda cha vigae cha Goodwill kilichopo mkoa wa Pwani, tumeshafikisha bomba kwenye kituo cha kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya kiwanda cha saruji cha Dangote vile vile miradi ya kuunganisha gesi asilia katika kiwanda cha Coca Cola, BIDCO na nyumba 67 katika jiji la Dar es Salaam pamoja na kutoboa bomba kuu la gesi asilia katika kijiji cha Mwanambaya kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kwa lengo la kutoa gesi ya kutosha na kusambaza kwenye viwanda vya Mkuranga kwa kuanza na Lodhia na Knauf.

Aidha akisisitiza kwenye kuongeza ugunduzi zaidi wa gesi asilia na mafuta ndugu Hans ameeleza kuwa “Tukiwa Shirika la Mafuta la Taifa pia tumeelekeza mikakati yetu kwenye kuhakikisha tunaongeza kiasi cha ugunduzi wa gesi asilia na pengine mafuta kwa kuendelea kufanya utafiti zaidi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ambapo kama sehemu ya mkakati kwa sasa tuna kitalu cha Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi, Kitalu namba 4/1b na 4/1c na Mnazi Bay Kaskazini pamoja na miradi hii ya kimkakati ambayo inafanywa na Shirika upo pia mradi unaotekelezwa na mwekezaji katika kitalu cha Ruvu ambae anaendelea na kufanya utafiti wa uhakiki wa kiasi cha gesi asilia katika kitalu hicho lengo kuu likiwa tuvuke pale kwenye futi za ujazo trilioni 57.55 zilizopo kwa sasa”

Sehemu ya baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalam kutoka TPDC na GASCO ambao waliweza kueleza mikakati ya TPDC katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha utafiti zaidi wa mafuta na gesi asilia unafanywa ili kuongeza uwepo wa rasilimali hizo kwa matumzi lakini pia usambazaji wa gesi asilia unafanywa kwa kasi kufikia wateja haswa viwanda
Sehemu ya baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalam kutoka TPDC na GASCO ambao waliweza kueleza mikakati ya TPDC katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha utafiti zaidi wa mafuta na gesi asilia unafanywa ili kuongeza uwepo wa rasilimali hizo kwa matumzi lakini pia usambazaji wa gesi asilia unafanywa kwa kasi kufikia wateja haswa viwanda

Aidha kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri ndugu Deodatus Balile ameipongeza TPDC kwa kuendesha warsha hiyo ambayo imeongeza uelewa mkubwa wa gesi asilia kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.

“Niwapongeze kwa kuendesha mafunzo haya kwakweli ni muhimu kama mlivyoona kuwa baadhi yetu bado hatuelewi masuala mengi ya sekta hii na ndio maana hata maana ya Mkondo wa Juu na Mkondo wa Chini katika Gesi na Mafuta imekuwa ikileta mkanganyiko kati yetu hivyo mnapaswa mfanye zoezi hili kuwa endelevu ili wahariri na waandishi waelewe haswa kiundani masuala ya mikataba, sheria zinazosimamia sekta hii pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na TPDC na matumizi na manufaa ya gesi asilia” ameongeza Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri.

Aidha Ndugu Balile ameshauri kuwa TPDC inapaswa kuunda kundi la waandishi wa habari ambao mtawajengea programu maalum ya elimu ya sekta kwa kuwapeleka kwenye maeneo ya uzalishaji, utafiti na uchimbaji pamoja na kuwapa mafunzo ya sheria, mikataba na masuala mengine ya sekta hii ambao hawa watakuwa mabalozi wenu upande wa vyombo vya habari” alifafanua ndugu Balile.


Comments