Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi Washika Kasi


Mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani,  Tanga unaendelea kushika kasi,  baada ya kukamilika kwa taratibu za awali za mradi huo.

Akizungumza kwenye kipindi cha Jambo Tanzania  kinachorushwa na TBC, Mratibu wa mradi Bwana Asiadi Mrutu amesema,  kwa sasa kinachoendelea ni kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo na kuandaa vituo vikubwa na vidogo vitakavyotumika kwenye ujenzi.

Amesema mradi huo utapita katika Mikoa 8, Wilaya 24 huku wananchi wa Mkoa wa Kagera pekee wakilipwa takribani shilingi bilioni 7 kama fidia, baada ya  kupisha mradi huo ambapo kutajengwa kambi  namba 5 na 6 na kituo cha kusukuma mafuta kimoja.

Uganda imegundua mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5,  huku EACOP ikianza kuzalisha zaidi ya mapipa bilioni moja.

Makadirio ya mapato yatakayopatikana kutokana na mradi huo ni takribani shilingi trilioni 2.3.

Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima,  Uganda hadi Chongoleani, Tanga kwa upande wa Tanzania  litakuwa na urefu wa kilomita 1,147 ambapo inatarajiwa kuzalisha ajira elfu 10 hadi elfu 15 kwa Watanzania.

Mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki ni mradi wa kimkakati wa Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),  unaotarajiwa kutumia miezi 36 hadi kukamilika kwake na unatajwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

Hadi kukamilika kwake, mradi huo unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani bilioni 5.1.