TPDC YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA KIJAMII KINYEREZI NA KIBITI

Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi.  Marie Msellemu akikabidhi hundi ya kiasi cha shillingi Milioni 22 kwa Mkuu wa Shule ya Msingi Kinyerezi Mwalimu Mwl. Pendaman Kajiru

Shirika la Petroli  Maendeleo ya Tanzania (TPDC) limeendelea na mchakato wa kuwajibika kwa jamii na kuendelea kuimarisha huduma mbalimbali zinazowagusa wananchi moja kwa moja kama elimu, afya, maji na utawala bora, ambapo kupitia Sera ya uwajibikaji maarufu kama ‘Corporate Social Responsibility’ (CSR), imeweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 22 katika Shule ya msingi Kinyerezi Dar es salaam kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Katika hafla ya kukabidhi hundi ya fedha hizo shuleni hapo, Meneja mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu alisema kuwa TPDC ni wadau wa elimu na Shirika linaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Joseph  Pombe Magufuli, katika suala zima la elimu bure na hivyo kuamua kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira tulivu na salama.

“TPDC ni wadau wa elimu, na tulipoletewa maombi ya kuchangia ujenzi wa madarasa katika shule hii ya msingi hapa Kinyerezi hatukusita kwani ni majirani zetu, kwani tumeendeleza falsafa ya ujirani mwema kama tunavyofanya kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo napo tumewekeza miundombinu ya gesi asilia”

Mgeni rasmi wa shughuli ya kukabidhi hundi ya fedha hizo alikuwa Bibi Sophia Mjema, ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Ilala, Bi. Sheila Lukuba. Akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu Wilaya, Bi Lukuba  aliishukuru TPDC kwa kuona umuhimu wa kutoa mchango huo katika Shule hio kwa lengo kuu la kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Bi.Sheila Lukuba akihutubia hadhara katika tukio la kukabidhi hundi S/M Kinyerezi.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Bi.Sheila Lukuba akihutubia hadhara katika tukio la kukabidhi hundi S/M Kinyerezi.

“Naipongeza na kuishukuru sana TPDC kwa kuona umuhimu wa kurudisha asilimia kwa jamii inayowazunguka kwa kutoa fedha za kujenga madarasa kwani itapunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa.” alisema Bi. Lukuba.

Hata hivyo, alihamasisha makampuni na taasisi zingine kuiga mfano wa TPDC na kujitokeza kutatua au kupunguza changamoto zilizopo mashuleni ili wanafunzi wasome katika mazingira bora huku pia akisisitiza wanafunzi kujikita katika kusoma ikiwa wadau wanafanya jitihada nyingi ili waweze kupata mazingira bora ya elimu.

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hio Mwl. Pendaman Kajiru aliishukuru TPDC kwa mchango wa ujenzi wa madarasa kwani kulingana na idadi ya wanafunzi shuleni hapo mchango huo utapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuahidi kutendea haki fedha hizo kwa  kujenga madarasa yenye hadhi .

“Napenda kushukuru uongozi wa TPDC kwa mchango wa Milioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwani  tuliwaomba na hawakusita kutusaidia na msaada huu umetatua kero kubwa ya wanafunzi kubanana katika madarasa kwani wanafunzi ni wengi.” Alisema Mwl. Kajiru.

Vilevile, Afisa Elimu wa kata ya Kinyerezi Bi. Mercy Mtei alishukuru uongozi mzima wa TPDC kwa kuwajengea madarasa kwani kulikua na uhaba mkubwa wa madarasa katika shule za kata kinyerezi ambapo alieleza kwamba uhaba wa madarasa ulipelekea idadi ya wanafunzi 90 kutumia darsa kwa siku moja.

Wakati huo huo katika jitihada za kuinua elimu, TPDC ilikabidhi hundi ya kiasi cha shillingi Milioni 10 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg. Gulam Kifu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Bungu “B” Wilayani Kibiti.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg.Gulam Kifu akikabidhiwa hundi ya shilingi Milioni 10 na Meneja Mawasiliano TPDC Bi. MarieMsellemu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji Bungu B.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Ndg.Gulam Kifu akikabidhiwa hundi ya shilingi Milioni 10 na Meneja Mawasiliano TPDC Bi. MarieMsellemu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji Bungu B.

Akizungumza  katika tukio  hilo Ndg. Kifu aliishukuru TPDC kwa mchango waliotoa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya serikali ya kijiji kwani jengo linalotumika sasa ni chakavu na hatarishi kwa usalama wa watumishi. Zaidi pia alisisitiza Kamati ya ujenzi kutumia fedha hizo kwa kazi iliokusudiwa.

 

 


Comments