Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema hadi sasa tayari magari 2,000 yameunganishwa na mfumo wa kutumia gesi asilimia huku nyumba 1,511 zikitumia gesi hiyo kama nishati ya kupikia.
Pia taasisi zaidi ya 10 na viwanda 56 zimeunganishwa kwenye matumizi ya nishati hiyo ambayo inachangia zaidi ya asilimia 50 ya umeme kwenye gridi ya Taifa.
Unafuu wa matumizi ya gesi asilia kwenye magari unabainishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) matumizi ya gesi asilia huokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 50 ya gharama mtu anazotumia kwenye dizeli na petroli.
Kwa mfano, mtungi wa kilogramu 15 wa CNG hujazwa kwa Shilingi 23,000 na hutembea wastani wa kilometa 250 kwa gari aina ya Toyota IST ambazo zingegharimu wastani wa Shilingi 70,000 kwa mafuta.
Hayo yameelezwa leo Agosti 15,2024 Jijini Dar es Salaam na Mhandisi wa TPDC Angelindile Marandu kupitia Semina ya Viongozi wa Dini na Madiwani wa Mkoa wa Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwajengea uelewa wa masuala yanayohusu nishati ya gesi.
“Gesi asilia inatumika kama nishati ya kupashia joto kwenye uzalishaji viwandani ambapo tayari tumeunganisha viwanda 56,pia gesi hii inatumika kama malighafi kuzalisha mbolea na bidhaa nyiginezo,”amesema Marandu.
Awali akifungua mafunzo kwa Viongozi hao wa Dini na Madiwani, Mkuu wa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amewasisitiza viongozi hao kuwa mabalozi wazuri kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya usafirishaji gesi asilia.
Aidha, amelipongeza Shirika la TPDC kwa kutumia Shilingi bilioni 1.8 kurejesha kwa jamii zilizo pembezoni mwa miundombinu ya gesi hiyo na kuliomba kuendelea kufanya hivyo, wananchi waone umuhimu wa kulinda miradi hiyo.
“Miradi mingi ina dhamira kubwa ya kukuza maendeleo ya taifa. Miezi michache iliyopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Reli ya Kisasa (SGR) ambayo leo imekuwa gumzo ukanda wa Afrika na ina matumizi makubwa ya umeme,”amesema Chalamila.
Akizungumzia mpango mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Chalamila alihamasisha umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo ambapo Serikali itahakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
“Ukiihujumu miundombinu kwa ujumla wake unakwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha gesi nyingi inawafikia walaji na pengine kufunga miundombinu ya namna hiyo.
“TPDC hufanya semina hizi kila mara kuwaongezea Viongozi uwezo, mpeleke ujumbe kwa wananchi katika maeneo ambayo miundombinu imepita, isiharibiwe na baadhi ya watu ambao uelewa wao siyo mkubwa,” amesema Chalamila.
Naye, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TPDC, Bw.Francis Mwakapalila akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mussa Makame, amesema semina hiyo ililenga kuwapa fursa ya kujifunza na kuelewa zaidi kuhusu gesi asilia na kuwakumbusha majukumu ya Shirika hilo.
Alieleza kuwa jukumu la msingi la TPDC ni kufanya tafiti, uendelezaji na usafirishaji wa gesi asilia nchini na kubainisha kuna miradi ya kimkakati 19, kati ya hiyo tisa ipo chini ya Wizara ya Nishati na minne ipo chini ya TPDC, ikiwemo mradi wa gesi ya LNG, bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, nchini Uganda hadi Tanga na utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Mnazibay Kaskazini.
Mwakapalila amesema shirika hilo linajipanga kuongeza matumizi ya gesi asilia kwa kujenga kituo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es salaam, kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi.
Kwa upande wa Viongozi walioshiriki semina hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Amani Kinondoni, Majaliwa Selemani, aliishukuru TPDC kwa semina hiyo na kuahidi watakuwa mabalozi wazuri kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu hiyo na kutunza mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia na kupanda miti.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment