DC MWANZIVA AIPONGEZA TPDC KUSHIRIKI MAONESHO YA NANENANE KANDA YA KUSINI
DC MWANZIVA AIPONGEZA TPDC KUSHIRIKI MAONESHO YA NANENANE KANDA YA KUSINI
Imewekwa: 04 August, 2025

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva, amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuwa miongoni mwa Taasisi za Serikali zinazoshiriki kikamilifu maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (NaneNane), Kanda ya Kusini. Pia amelipongeza Shirika kwa kutumia maonesho hayo kuelimisha umma juu ya utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi asilia. Pongezi hizo amezitoa tarehe 02.08.2025 alipotembelea banda la TPDC kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo, vilivyopo Manispaa ya Lindi.
Akizungumza bandani hapo Mwanziva alisema, TPDC ni Shirika la Kimkakati ambalo sehemu kubwa ya shughuli zake za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia unafanyika katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Hivyo, naipongeza sana TPDC kwa kushiriki kikamilifu maonesho haya ambapo, watu wa Kusini watapata fursa ya kujifunza namna Shirika letu linavyotekeleza miradi ya gesi yenye tija kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.”
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuiwezesha TPDC kutekeleza miradi mikubwa ya mafuta na gesi asilia, na hapa tumemsikia Mtaalamu akizungumzia utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Lindi na Mtwara. Haya ni mafanikio makubwa ambayo Wananchi wanapaswa kujulishwa,” aliongeza Mhe. Mwanziva.
Katika hatua nyingine, Mtaalamu wa Miamba (Palnologist) kutoka TPDC Bw. Innocent Mvamba alitoa ufafanuzi wa majukumu na miradi inayotekelezwa na TPDC mbele ya Mhe. Mwanziva pamoja na ujumbe wake.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015, TPDC inatambulika kama Shirika la Mafuta la Taifa ambalo linatekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa mafuta na gesi nchini. Mpaka sasa Nchi yetu imefanikiwa kugundua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.54 kwenye kina kirefu cha bahari na nchi kavu. Aidha, TPDC inaendelea na miradi mbalimbali ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Eyasi Wembere, Lindi-Mtwara, M nazi Bay Kaskazini, SongoSongo Magharibi, na kitalu cha 41B/41C,” alisema Mvamba.
Mvamba aliongeza kuwa, “miradi mingine inayotekelezwa na TPDC ni usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya viwandani, majumbani na kwenye magari. Mathalani, mpaka sasa, mtandao wa usambazaji wa gesi asilia umeunganisha jumla ya viwanda 57 nyumba 1512, pamoja na kuhudumia magari zaidi ya 5000 na bajaji zaidi ya 5000. Vilevile, TPDC kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuunganisha nyumba 470 na Taasisi 1 katika Kata ya Mnazi Mmoja-Lindi na nyumba 530 katika ijiji cha Kisemvule-Mkuranga” Alifafanua Bwa. Mvamba
Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka huu yanaendelea katika Kanda mbalimbali hapa nchini (ambapo kwa Kanda ya Kusini yanafanyika katika viwanja vya ngongo Manispaa ya Lindi) huku yakiwa na kauli mbiu “Chagua Viongozi bora kwa Maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi 2025.