Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

MASLAHI MAPANA YA NCHI YANAZINGATIWA UTEKELEZAJI WA MRADI WA EACOP – DKT. MATARAGIO

Imewekwa: 29 July, 2025
MASLAHI MAPANA YA NCHI YANAZINGATIWA UTEKELEZAJI WA MRADI WA EACOP – DKT. MATARAGIO
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sekta ya Mafuta na Gesi Wizara ya Nishati, Dkt James Mataragio, amesema utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unazingatia maslahi mapana ya nchi ikiwemo upatikanaji wa ajira kwa wazawa, kuongezeka kwa pato la Taifa na ushirikishwaji wa kampuni za wazawa kutoa huduma kwenye utekelezaji wa mradi wa EACOP. . Akiwa kwenye kiwanda cha kuweka mifumo ya upashaji na utunzaji wa joto(Thermal Insulation System ) Dkt.Mataragio alijionea namna mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga yanavyoandaliwa na kuwekwa teknolojia maalumu ya kudhibiti kutu eneo la Sojo Wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora. ‘’ Wizara ya Nishati ndio mwenye dhamana ya kusimamia maslahi ya Serikali chini ya TPDC na tumeridhika na maendeleo ya utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia sheria na mikataba iliyopo, ambapo mpaka sasa fedha zote za mradi wa EACOP zimepatikana kwa asilimia mia moja,’’ amesema Dkt. Mataragio Ameongeza kuwa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki unaendelea kwenye mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara, na Tanga na utahusisha pia ujenzi wa vituo 4 vya kuongeza msukumo wa mafuta (Pump Stations) na vituo viwili vya kupunguza msukumo wa mafuta (Pressure reduction Stations) ambao umekamilika kwa asilimia 55. ‘’Ujenzi wa bomba la Mafuta ghafi la EACOP kwa sasa umefikia asilimia 65 na utagharimu kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 5.65 na jambo la kufurahisha ni kwamba ajira za wazawa takribani 9,194 zimezalishwa katika kipindi cha ujenzi wa mradi na kati ya hizo asilimia 75 zimenufaisha wazawa,’’ amesistiza Dkt. Mataragio Amesema mpaka sasa jumla ya shilingi bilioni 60 zimepatikana kutokana na manufaa ya utekelezaji wa mradi wa EACOP ikiwemo  makusanyo ya pango la ardhi, ushuru wa huduma na usajili wa vibali mbalimbali kwenye Halmashauri. Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki unatekelezwa na nchi mbili za Tanzania na Uganda ambapo kila moja ina hisa asilimia 15, ambapo UNOOC ya China asilimia 8 na Total Energies asilimia 62 ambapo mradi unatarajia kukamilika mwezi Julai, 2026.