Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

KATIBU MKUU NISHATI ATOA WITO WA UONGOZI UNAOACHA ALAMA KWA MENEJIMENTI YA TPDC

Imewekwa: 28 July, 2025
KATIBU MKUU NISHATI ATOA WITO WA UONGOZI UNAOACHA ALAMA KWA MENEJIMENTI YA TPDC
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ametoa wito kwa Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni zake tanzu kuongeza kasi na bidii katika utendaji kazi, akisisitiza umuhimu wa uongozi wenye matokeo chanya na unaoacha alama ya kudumu kwa taifa. Akizungumza katika kikao cha Menejimenti ya TPDC kilichofanyika Jijini Arusha kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango ya mwaka wa fedha 2024/2025 na kuweka mikakati ya mwaka 2025/2026, Mha. Mramba alikumbusha kuwa kila kiongozi ana kipindi kifupi cha kuhudumu, hivyo ni muhimu kuhakikisha muda huo unatumiwa kwa ufanisi na tija. “Uongozi si wa milele, kila mmoja ana muda wake. Ni muhimu kuhakikisha muda huo unatumika vizuri ili kuleta matokeo chanya yatakayobaki kama alama kwa taifa,” alisisitiza Mramba. Aidha, alibainisha kuwa TPDC inayo nafasi ya kipekee ya kuandika historia kutokana na ukubwa na umuhimu wa miradi inayosimamia katika sekta ya mafuta na gesi. Alitoa mfano wa mradi wa utafutaji mafuta na gesi katika Kitalu cha Eyasi-Wembere, akihimiza kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufanikisha mafanikio ya kihistoria. “Ongezeni kasi katika utekelezaji wa miradi yenu, hasa ule wa utafutaji mafuta na gesi wa Eyasi-Wembere. Siku moja tukigundua mafuta, mtakuwa na cha kujivunia kama viongozi wa kizazi hiki – kwamba mliweka msingi wakati wa uongozi wenu,” alisema Mramba. Katika kikao hicho, washiriki walipitia mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza, na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha utekelezaji wa mipango unakwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini. Kauli ya Katibu Mkuu imepokelewa kama chachu na msukumo mpya kwa Menejimenti ya TPDC kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo, na kujituma kwa lengo la kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi inachangia kikamilifu maendeleo ya taifa.