Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

TPDC NA KAMPUNI YA ENERGETECH TANTEL KUJENGA MITAMBO MIDOGO YA GESI KIMIMINIKA (MINI LNG PLANT)

Imewekwa: 07 July, 2025
TPDC NA KAMPUNI YA ENERGETECH TANTEL KUJENGA MITAMBO MIDOGO YA GESI KIMIMINIKA (MINI LNG PLANT)
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Energetech-Tantel zimefikia makubaliano ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MOU) itakayowezesha ujenzi wa mitambo midogo ya gesi kimiminika ‘‘Mini LNG Plant’’ itakayowezesha upatikanaji rahisi wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya mipaka ya Tanzania. Tukio hilo muhimu limefanyika Jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati nchini Tanzania Bw. Goodluck Shirima, akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko. Utiaji saini huo unakwenda sanjari na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kama Kituo kikuu cha nishati kikanda, ikiwamo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hati hiyo ya Makubaliano  inaeleza mpango kazi kabambe wa miaka miwili unaojumuisha tafiti, vibali muhimu, uhandisi wa kina, upatikanaji wa fedha, na hatimaye, uzalishaji wa kimiminika cha gesi (LNG) ambapo uzalishaji wa kwanza wa LNG unatarajiwa kuwa ndani ya miezi 12 ijayo. Mradi huu bunifu unalenga kutumia rasilimali ya gesi asilia iliyopo nchini ili kuwezesha urahisi wa upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na rafiki kwa mazingira kwa watumiaji mbalimbali wakiwemo viwanda, vyombo vya usafiri, majumbani, umeme na taasisi mbalimbali. Mradi huo, unaokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 80–100, kwa awamu ya kwanza utahusisha ujenzi wa mtambo ya Mini LNG wa kisasa utakaobadili gesi kuwa kimiminika ili iweze kusafirishwa katika mitungi maalumu hadi kwenye masoko ndani na nje ya nchi. Uzalishaji wa awali unakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo milioni 20 hadi 30 kwa siku, na uwezo mkubwa utawezesha uzalishaji hadi futi za ujazo zaidi ya milioni 100 kwa siku. Chini ya masharti ya mkataba huo, Energetech-Tantel itaongoza vipengele vya ufadhili, uhandisi, na usambazaji wa bidhaa za mwisho wa mradi, ikilenga kutoa nishati mahali panapohitajika zaidi. Aidha, TPDC itatoa msaada muhimu katika upelekaji wa gesi kwa ajili ya kusindikwa na kuwa kiungo cha ushirikiano na mamlaka za serikali, ikiwa ni pamoja na taratibu muhimu za vibali. Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamishna wa Petroli na Gesi Bw. Goodluck Shirima alisema, "Uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu kwa kutoa suluhisho linaloweza kutumika kuendeleza viwanda kwa Tanzania, kipaumbele kikiwa kuendeleza matumizi ya ndani ya gesi. Mara baada ya kuanza kazi, kaya na viwanda vya Tanzania vitafaidika na nishati safi ya gesi, na hivyo kupunguza gharama katika matumizi ya nishati." Naye, Mkurugenzi Mtendaji, TPDC Bw. Mussa Makame alisema, " TPDC inashabikia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unaotoa suluhisho kwa Watanzania." Aidha, Makame alisema kwamba mkataba huo umelenga kutumia rasilimali kuwezesha nishati safi na kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na nchi za jirani pia. “Tunajivunia kushirikiana na Energetech-Tantel katika uzalishaji wa gesi kwani ni muhimu kwa mkakati wetu." Afisa Mtendaji Mkuu wa Energetech-Tantel. Bw. Alistair Naiken alisema kuwa mkataba huo sio wa ushirikiano tu ushirikiano, bali ni ahadi ya pamoja ya kubadilisha sekta ya nishati Tanzania. "Tunajenga suluhisho la nishati halisi ambazo zitabadilisha jamii, tukitoa gesi mahali na kwa wakati tukiipeleka inapohitajika zaidi, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati hii kwanza, hasa wateja wa viwandani, kama nishati safi."  Rais wa Tantel Holdings, Bw. Daniel Gabai, akitoa maoni yake alisema: "Tanzania ni nchi yenye matumaini zaidi Afrika Mashariki. Katika Tantel Holdings, hatuwekezi tu katika uwezekano bali katika watu, tukikumbatia changamoto kubwa za miundombinu.  “Tunaamini Tanzania itakuwa nguvu inayoongoza kwa ukuaji barani Afrika katika muongo ujao, na mradi huu utakuwa mradi bora zaidi wa nishati safi barani, ukiwahudumia soko la ndani na kikanda."