Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

TPDC YATEKELEZA PROGRAMU YA UELIMISHAJI JAMII KUHUSU MRADI WA UCHUKUAJI WA TAARIFA ZA MITETEMO MIKOA YA LINDI NA MTWARA

Imewekwa: 04 August, 2025
TPDC YATEKELEZA PROGRAMU YA UELIMISHAJI JAMII KUHUSU MRADI WA UCHUKUAJI WA TAARIFA ZA MITETEMO MIKOA YA LINDI NA MTWARA
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetekeleza programu muhimu ya utoaji elimu kwa wadau na jamii zinazopitiwa na mradi wa uchukuaji wa taarifa za mitetemo (3D seismic survey) katika Kitalu cha utafutaji wa mafuta na gesi asilia cha Lindi-Mtwara. Zoezi hili la elimu na uhamasishaji linalenga kuwajengea uelewa wadau na jamii juu ya umuhimu wa mradi na kuhamasisha ushirikiano katika utekelezaji wake. Akizungumza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa Mradi wa Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia wa Kitalu cha Lindi-Mtwara, Dkt. Shaidu Nuru ambaye pia ni Mjiolojia Mwandamizi kutoka TPDC, alisema zoezi la utoaji elimu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi ambapo TPDC inalenga kuwafikia wadau wote muhimu kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji na Kitongoji, lengo hasa likiwa ni kutoa elimu ya umuhimu wa mradi na kuhamasisha ushirikiano wa wadau. Aidha, Dkt. Shaidu alieleza kwamba “mradi huo, unatekelezwa na TPDC kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi wa Julai, 2025, na unategemea kutumia teknolojia ya kisasa ambayo hujumuisha matumizi ya magari maalum yanayotoa mitetemo midogo pamoja na vipokezi vinavyopokea mitetemo hiyo inaporudi kutoka ardhini. Teknolojia hiyo huwasaidia wataalamu kupata picha ya kina ya miundo ya kijiolojia chini ya ardhi, hivyo kusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu maeneo bora ya kuchimba na kupunguza gharama na hatari katika shughuli za utafutaji.” Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC Bw. Ally Mluge, alibainisha kuwa, TPDC imekuwa ikitekeleza programu za uelimishaji jamii kuhusu umuhimu wa miradi na shughuli za Shirika katika kukuza uchumi wa Taifa. Vilevile, alieleza kuwa ushirikishwaji huu husaidia kurahisisha utekelezaji wa shughuli au miradi ya TPDC. Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Vijiji Mkoa wa Mtwara ndugu Hamisi Chikandanga, aliipongeza TPDC kwa kuandaa programu hii ya elimu. Alibainisha kuwa imewasaidia wananchi kuelewa juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali kupitia TPDC. Pia aliliomba Shirika la TPDC kuendelea na programu kama hizo katika utekelezaji wa miradi mingine ijayo. Programu hii ya uelimishaji jamii inahusisha Vijiji 30 vinavyopitiwa na mradi huo, ambapo Vijiji 22 viko Mtwara (ambavyo ni Hiari, Msijute, Lokonde, Mayanga, Nangumi, Utende, Namgogoli, Ndumbwe, Mnyundo, mbuo, Mwatehi, Changarawe, Muungano, Mwembetogwa, Mkajuni chini, Mkwajuni juu, Lyowa, Manamawa, na Namkapi) na Vijiji 8 viko Lindi (ambavyo ni Mtegu, Sudi, Madangwa, Nachunyu, Mmumbu, Navanga, Mongomoho na Shuka). Aidha, Kukamilika kwa zoezi hilo la elimu kunaashiria hatua muhimu katika kuhakikisha uwazi na ushirikishwaji wa jamii katika miradi ya maendeleo ya nishati, huku ikijenga msingi imara wa ushirikiano kati ya TPDC na wananchi.