SHILINGI BILIONI 120 KUTEKELEZA UJENZI WA BOMBA LA KUSAFIRISHA GESI ASILIA KUTOKA NTORYA HADI MADIMBA MKOANI MTWARA
SHILINGI BILIONI 120 KUTEKELEZA UJENZI WA BOMBA LA KUSAFIRISHA GESI ASILIA KUTOKA NTORYA HADI MADIMBA MKOANI MTWARA
Imewekwa: 07 July, 2025

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema litatumia takribani shilingi bilioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la gesi asilia kutoka Ntorya hadi Madimba mkoani Mtwara.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 3,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Bw. Mussa Makame katika hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi wa bomba hilo na Kampuni ya China ya CPP na CPTDC kwa kipindi cha miezi 12.
"Bomba litakalojengwa litakuwa na inchi 14 na uwezo wa kusafirisha gesi ya futi za ujazo milioni 140 kwa siku, kiwango hiki cha gesi kinauwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 700,mradi huu ni muhimu kwa watumiaji gesi asilia,’’ amesema Makame.
Mnazi Bay na Songosongo zimekuwa za muda mrefu, Songosongo imezalisha gesi kwa miaka 20, Mnazibay miaka 18 na kiwango cha gesi kimeshaanza kupungua hivyo tunahitaji vyanzo vipya,"amesema Makame.
Makame amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa Bomba, ambapo kazi hii itatekelezwa na TPDC na kazi ya uchimbaji wa visima itatekelezwa na Kampuni ya ARA Petroleum kazi ambayo itakamilika kwa miezi 12.
Katika utekelezaji wa ujenzi wa bomba hilo,Makame amesema vijiji 11 vitapitiwa na mradi huo na tayari tathmini ya mazingira imefanyika pamoja na malipo ya fidia kwa watakaopitiwa na mradi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CPP ya China Bai Zhengshuai amesema mradi huo wataukamilisha kwa wakati na watazingatia Sheria za nchi wakati wa ujenzi wa bomba hilo.
"Mradi huu tutautekeleza kwa wakati na tutafuata sheria za nchi,mradi huu kwetu tutaufanya kwa ufanisi ili kuendeleza ushirikiano wetu,"amesema Bai.