Angola na Tanzania Zajadiliana Ushirikiano Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia 


Dar es salaam.

Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Sandro Renato Agostinho De Oliveira

amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli

Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio kuangazia maeneo mbalimbali ambayo

Angola na Tanzania wanaweza kushirikiana hususan katika Sekta ya mafuta na gesi

asilia.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sandro alieleza nia ya Serikali ya Angola

kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika sekta ya mafuta na gesi ambayo

Angola ina uzoefu wa miaka mingi, “Angola tuna uzoefu wa miaka mingi katika sekta hii

ya mafuta na gesi na tunaamini kwa kushirkiana na Tanzania tunaweza kubadilishana

uzoefu na ujuzi katika tasnia hii” alieleza Balozi Sandro. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alieleza hatua

mbalimbali ambazo Tanzania imepiga katika tasnia hii ikiwemo ujenzi wa miundombinu

ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia pamoja na kuwa na matumizi ya gesi asilia

ambapo hadi sasa asilimia 62% ya umeme nchini unazalishwa na gesi asilia.

‘’Tunatambua kuwa Angola wamepiga hatua kubwa katika Sekta hii na tumezungumza

na Mheshimiwa Balozi kuona Kampuni zetu za Mafuta yaani TPDC kwa upande wa

Tanzania na Sonangol  kwa upande wa Angola zinakuwa na ushirikiano wa karibu ili

kubadilisha uzoefu na ujuzi katika tasnia hii,’’ alieleza zaidi Dkt. Mataragio.