Bodi ya TPDC Yaanza Kazi, Yafanya Ziara Mtwara na Lindi
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inayoongozwa
na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue imefanya ziara ya kikazi
kutembelea miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika mikoa ya
Lindi na Mtwara.
Akiongea baada ya kuona kazi za ukusanyaji takwimu za mtetemo kwa mfumo wa 3D
katika kitalu cha Ruvuma kinachoendeshwa na ARA Petroleum Tanzania, Balozi Sefue
alisema “Matumizi ya gesi asilia hapa nchini yameendelea kukuwa siku baada ya siku
hivyo kazi inayofanyika katika kitalu hiki inalenga kuongeza uzalishaji wetu wa gesi asilia
ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mahitaji yake”. Balozi Sefue alioneshwa kuridhishwa na
kazi zinazoendelea katika kitalu cha Ruvuma na kuwaasa ARA Petroleum Tanzania
kuendelea na kasi hiyo ili kuendana na uwekezaji unaofanyika ndani ya nchi ambao kwa
kiasi kikubwa unahitaji nishati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alieleza namna
TPDC kama mwenye leseni zote za vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi hapa nchini
anavyoshirikiana na wawekezaji katika mkondo wa juu kuhakikisha shughuli za utafutaji
na uendelezaji wa rasilimali hizi unaendelea kwa kasi. Dkt. Mataragio alisema “TPDC kwa
kushirikiana na wawekezaji tumeendelea kufanya kazi mbalimbali za kitaalam zenye lengo
la kuhakikisha kuwa tunaendeleza sekta yetu ya gesi na mafuta na kuendana na
ongezeko la mahitaji ya gesi asilia ndani na nje ya nchi”.
Aidha, Meneja Mkuu wa ARA Petroleum Tanzania, Ndg. Erhan Saygi alieleza mategemeo
yao kama kampuni ni kuzalisha gesi katika visima vya Ntorya 1, Ntorya 2 pamoja na
Chikumbi 1 ambacho kiko katika maandalizi ya awali. “Tumepanga kukamilisha kazi ya
ukusanyaji wa takwimu za mtetemo mwezi Novemba na kuanza kuchimba kisima cha
Chikumbi 1 ambacho kitakuwa cha tatu katika kitalu hiki mapema mwaka 2023”. Ndg.
Erhan pia alieleza mategemeo yao ni kuzalisha futi za ujazo milioni 60 kwa simu
(60mmscfd) kwa kuanzia na uzalishaji utaendelea kukuwa kadri mahitaji ya gesi
yatakavyokuwa.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment