Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) imefanya ziara ya kikazi katika Kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha joto mabomba ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kilichopo eneo la Sojo Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.
Akizungumza katika Ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Japhet Hasunga (Mb) alisema kuwa ziara ya kamati hiyo ililenga kuangalia mambo matatu ambayo ni; kuangalia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali zote mbili za Tanzania na Uganda pamoja na mwekezaji kuona ni hatua gani imefikiwa katika kukamilisha kiwanda cha kuweka mfumo wa upashaji joto mabomba lakini pia kuona fedha ambazo zimepitishwa na Bunge zimetumika, kujifunza namna ambavyo kiwanda kinajengwa na kitatoa mchango gani katika Taifa, ajira mbalimbali ambazo zimetengenezwa na mradi kwaajili ya Watanzania na namna ambavyo jamii yote inayozunguka mradi itanufaika. “Kupitia ziara yetu hii niseme tu kuwa tumeridhishwa na namna ambavyo fedha zilizopitishwa na Bunge na kulipwa na Serikali kwaajili ya mradi huu zimetumika,” alisema Hasunga.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai alisema kuwa kuwepo mradi wa bomba la mafuta katika Wilaya ya Nzega kumetoa nafasi kubwa za ajira kwa vijana pamoja na kuboresha miradi ya kimaendeleo na maisha ya Wananchi wanaoishi jirani na mradi. “Mradi umechangia utoaji wa ajira kwa Wananchi wetu ambapo zaidi ya asilimia 98 ya wafanyakazi walioajiriwa katika kiwanda kwa kada zisizohitaji ujuzi wa juu wanatoka katika maeneo ya jirani na mradi,” alisema Naitapwaki.
Mhe. Naitapwaki aliendelea kwa kusema kuwa Kata ya Igusule ambapo ndipo kinajengwa kiwanda imepata kuendelea kupitia biashara mbalimbali ambazo zinafanyika kwenye mradi, uwepo wa makazi bora yaliyojengwa na mradi, kuongezeka na kuimarika kwa suala zima la ulinzi pamoja na kutolewa kwa elimu ya ufugaji wenye tija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bwana Mussa Makame alisema kuwa ujenzi wa Kiwanda hicho umekamilika kwa asilimia 61 na mabomba yamekwishaanza kuwasili. “Mabomba yenye uwezo wa kujenga umbali wa kilomita 300 tayari yamekwishafika katika eneo hili na terehe 26.03.2024 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kuzindua rasmi kiwanda hiki na tunategemea mwezi wa nne kianze kufanya kazi,” alisema Makame.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment