Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio,amefanya ziara ya kikazi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuzungumza na Menejimenti ya TPDC lengo likiwa ni kujenga uhusiano wa karibu na kuboresha ushirikiano katika sekta ya nishati. Ziara hiyo imefanyika katika Ofisi za TPDC zilizopo Jengo la Benjamin Mkapa- Posta Jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ilijikita katika kuelewa zaidi namna Shirika linavyofanya kazi na changamoto linazokabiliana nazo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Aidha ziara ililenga kupata ufahamu kuhusu shughuli za utafutaji, uendelezaji, uzalishaji na usambazaji wa nishati ya gesi asilia pamoja na huduma kwa wateja zinazotekelezwa na TPDC.
Aidha Dkt. Mataragio ameitaka TPDC kuweka ukomo wa muda (deadlines) kwa miradi yake yote inayotekeleza pamoja na ile inayotekeleza kwa ubia na wawekezaji. “Ni vizuri kuweka ukomo wa muda katika miradi yote pamoja na ile inayotekelezwa kwa ubia na wawekezaji ili kurahisisha ufuatiliaji na utekelezaji wake kwa wakati.”
Dkt. Mataragio pia amegusia umuhimu wa TPDC kuandaa mpango madhubuti wa usambazaji wa gesi asilia (Natural Gas Distribution Master plan) kwa matumizi mbalimbali katika harakati za Serikali kupunguza matumizi ya vyanzo chafuzi vya nishati.
Dkt. Mataragio aliwahakikishia Viongozi wa TPDC kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo katika sekta ya nishati hususan sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment