Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Serikali imejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia majumbani,viwandani na kwenye magari
Akizungumza alipotembelea banda la TPDC kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara amesema TPDC inaendelea kutekeleza miradi hiyo ya usambazaji gesi asilia katika maeneo mbalimbali hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi itaweza kuwafikia watumiaji wengi zaidi
Aidha Mramba amesema kuna Watanzania wanahitaji huduma zinazotolewa na kampuni tanzu ya TPDC -GASCO katika ujenzi wa vituo vya mafuta na vituo vya kujaza gesi kwenye magari (CNG) pamoja na namna bora ya usimamizi wa vituo hivyo .
‘’Wapo Wafanyabiashara wanajenga vituo vya mafuta lakini hawajui Mzabuni wa kuwajengea vituo wanampata wapi hivyo maonesho haya ni fursa kwa TPDC,GASCO na TANOIL kujitangaza zaidi,’’amesema Mramba.
Aidha amesisitiza kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi asilia majumbani na kwenye vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari ili kukuza ushiriki katika mchango wa uchumi wa nchi.
Mpaka sasa TPDC inashirikiana na sekta binafsi kujenga vituo 30 vya kujaza gesi katika Jiji la Dar es salaam, maeneo vitakapojengwa vituo hivyo ni maeneo ya Muhimbili, Kibaha, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Sinza, Mwenge, Goba, Mbezi Beach na Mbagala.
Vilevile, TPDC inatarajia kuleta magari ya kujaza gesi kwenye vituo kwa kutumia ,magari maalum ya kubeba gesi asilia.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment