Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhe. Balozi Ombeni Sefue amesema ujenzi wa Kituo mama cha gesi iliyoshindiliwa yaani Compressed Natural Gas (CNG) umefikia asilimia 33.5 na utakamilika mwezi Desemba.

Hayo ameyasema leo tarehe 21.08.2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kujionea maendeleo ya  ujenzi wa Kituo hicho kilichopo barabara ya Sam Nujoma eneo la Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Balozi Sefue amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo kutasaidia kutekeleza mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi ili kupunguza hewa ya ukaa inayochangia kuleta mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.

‘’Mojawapo ya vipaumbele vya TPDC ni kuhakikisha kwamba siku hadi siku maisha ya Watanzania, usafiri wa Watanzania, umeme wanaoutumia Watanzania na uzalishaji viwandani, kwa kadri inavyowezekana, unatumia gesi asilia ambayo ni safi kuliko nishati nyingine zinazotumika hapa nchini hivi sasa,’’amesema Balozi Sefue. 

Akizungumza kuhusu mipango mbalimbali ya Shirika amesema,  TPDC inatarajia kuleta vituo sita vinavyohamishika ambapo kila kituo kitakuwa na uwezo wa kujaza gari mbili kwa wakati mmoja. Vituo hivi vitawekwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Dodoma na Manispaa ya Morogoro. Aidha, Kituo mama hicho    kitahudumia vituo vidogo vitakavyojengwa maeneo mbalimbali ya nchi ambayo hayana gesi inayosambazwa kwa njia ya  mabomba.

Vilevile, Balozi Sefue amewasisitiza  wamiliki wa viwanda katika Jiji la  Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam kuchangamkia fursa ya CNG kwaajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalishaji umeme na kuendeshea mitambo.

‘’Natoa wito kwa Watanzania kuendelea kuweka mifumo ya gesi asilia kwenye magari yao ama kununua magari yanayotumia gesi asilia kwa kuwa sasa gesi itakua ikipatikana kwa uhakika na urahisi zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.’’

Naye, Meneja Msimamizi wa Mradi wa CNG kutoka TPDC Mhandisi Aristides Katto amesema ujenzi wa mradi huo utagharimu shilingi Bilioni 14.55.Kituo hiki kitakuwa na uwezo wa kushindilia gesi kwenye magari matatu (3) ya kusafirisha gesi kupeleka mahali pengine pia kitakuwa na uwezo wa kujaza magari 1000 kwa siku.

Aidha, upekee wa Kituo hiki ni kwamba kitakuwa na pampu za kujaza gesi nne, na kila pampu itakuwa na nozeli mbili. Hivyo kutakuwa na nozeli nane zenye uwezo wa kujaza CNG kwenye gari nane kwa mara moja. Vilevile, kituo kitakuwa na pampu maalumu tatu za kujaza gesi kwenye magari maalumu ya kubebea gesi asilia tayari kwa kusafirishwa.