Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema tayari limeingia makubaliano na Kampuni mbili za kigeni kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kusafirisha gesi asilia katika nchi ya Uganda, Congo,Kenya na Zambia.

Kampuni ambazo zimeingia makubaliano na TPDC Mei 2024 ni ROSETTA kutoka nchi za Falme za Kiarabu na KS Energy ya Uturuki huku mkataba mwingine ukisainiwa na Kampuni ya ESSA ya nchini Indonesia kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea aina ya urea.

Hayo yameelezwa Septemba 13,2024 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC,Ahmad Massa wakati akifungua Semina ya Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam ambayo imeandaliwa na Shirika hilo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa taarifa sahihi kuhusu masuala ya mafuta na gesi.

“TPDC inampango wa kuuza gesi asilia katika nchi za jirani ambazo tayari Serikali ilishaingia makubaliano ya awali, nchi hizo ni Uganda, Kenya, Congo na Zambia ambapo gesi inaweza kufika kwa wateja hawa kwa njia ya bomba ama LNG/Mini LNG,”amesema Massa.

Kuhusu mkataba wa kuzalisha mbolea kupitia gesi asilia, Massa amesema mbolea itakayozalishwa itakuwa mkombozi katika sekta ya kilimo nchini mwetu lakini pia italifanya taifa letu kuwa tegemeo la mbolea katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Mbali na hayo, Massa ameeleza TPDC kwa kushirikiana na AR Petroleum wanatarajia kuanza uzalishaji wa gesi asilia  eneo la Ntorya kwa kuanza kuzalisha futi za ujazo milioni 60 za gesi asilia kwa siku na kupeleka kwenye Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani Mtwara.

“Vilevile tutaenda kufahamu utekelezaji wa mashirikiano na Sekta binafsi katika kukuza matumizi ya gesi asilia nchini ambapo hadi sasa TPDC imesharuhusu Kampuni binafsi zaidi ya 30 kujenga vituo vya gesi asilia iliyogandamizwa nchini (CNG) ili kuwezesha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini,”amesema Massa.

Akiwasilisha mada kwa Wandishi wa Habari, Mjiolojia Mwandamizi Idara ya Mkondo wa juu TPDC, Dkt. Shaidu Nuru amesema shughuli za uzalishaji gesi zilianza mwaka 2004 katika vitalu vya SongoSongo, Mnazi Bay mpaka hivi sasa visima virefu 96 vimechimbwa vikiwemo vya utafutaji na uzalishaji gesi asilia. 

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi Idara ya Mkondo wa Chini TPDC, Anthony Karomba alitaja matumizi ya gesi asilia yakiwemo asilimia 50 ya umeme unaozalishwa nchini unategemea gesi hiyo, huku viwanda 56 vikiunganisha na magari na bajaji zaidi ya 5,000 yakitumia gesi hiyo na nyumba 1,511 na taasisi 13 zimeunganishwa. 

Kuhusu utekelezaji wa Mpango wa matumizi ya nishati safi, Karomba amesema kwa miaka 10 ijayo asilimia 50 ya wakazi wa Dar es Salaam watakuwa wanatumia nishati safi.