Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felichesmi Mramba amewahakikishia watumiaji wa gesi asilia kwenye magari kuwa kadhia waliokuwa wakiipata kutokana na uhaba wa vituo vya kupata huduma hiyo itafikia ukomo kuanzia mwisho wa mwaka huu.
Ameyasema hayo leo tarehe 20.09.2024 wakati wa ziara yake fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Mama cha Kushindilia gesi asilia (CNG Mother Station) kinachojengwa na kumilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma.
“Kwa muda mrefu jijini Dar es Salaam tumekuwa na Kituo kimoja cha Ubungo Maziwa kikifuatiwa na kile cha Tazara na cha sasa hivi Kituo cha tatu ni kile cha Uwanja wa Ndege lakini kituo kinachojengwa hapa kitakuwa kikubwa zaidi kuliko vilivyopo kwa sasa kwahiyo uwepo na kukamilika kwa Kituo hiki mwishoni mwa mwaka basi zile foleni kwenye vituo vilivyopo sasa hazitokuwepo” ameeleza Mha. Mramba.
‘’Kwanza naomba nitoe rai kwa watanzania wanavyoona Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kama mnavyoona hapa nadhani ni wakati muafaka kwa watu mbalimbali na wenyewe kuwa tayari kubadilisha magari yao ili yaweze kutumia gesi asilia.’’
Akielezea huduma zitakazotolewa na Kituo hicho Mha. Mramba alibainisha kuwa Kituo kitakua na eneo la kujaza gesi kwenye magari makubwa ya kusambaza gesi asilia pamoja na vituo vya kuhamishika, kujaza gesi kwenye magari yanayotumia gesi asilia na kutakua na karakana ya kuweka mifumo ya gesi asilia kwenye magari.
Mha. Mramba amewasisitiza Wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwasababu imethibitika kitaalam kabisa ya kwamba ukitumia gesi asilia unaokoa zaidi ya 50% ya gharama ya mafuta, kwa mfano kwa mwezi gari yako inatumia shilingi laki mbili basi kwa kutumia gesi asilia utatumia chini ya shilingi laki moja.
Aidha, kwa upande wake Mha. Mwikwabe Mhono kutoka TPDC ameeleza kuwa mradi umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni kazi za ujenzi na kazi za uundwaji wa mitambo ambapo kwa upande wa kazi za ujenzi amebainisha kuwa zilianza mwishoni mwa mwezi wa sita na hadi sasa tayari ukamilifu wake umefikia 57% na kwa upande wa uundwaji wa mitambo ambao unafanyika nchini China tayari umefikia 99%.
Mradi wa ujenzi wa Kituo Mama cha CNG cha TPDC unaenda sambamba na ujenzi wa vituo vidogo vya hospitali ya Muhimbili na Kiwanda cha Madawa cha Kairuki kilichopo Kibaha.
Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha ukuaji wa matumizi ya gesi asilia nchini hata kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na bomba la gesi asilia.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment