Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya kujaza gesi kwenye magari katika vituo vya kujazia gesi asilia.

Ufafanuzi huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi Mhandisi Emmanuel Gilbert wakati akifanya mkutano na Waandishi wa Habari leo tarehe 03.10.2024 Jijini Dar es salaam.

Amesema changamoto ya upatikanaji wa gesi asilia kwenye magari inatokana na mapokeo ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari kuongezeka na hivyo kusababisha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya kujaza gesi kwenye vituo vya kujazia gesi.

Akieleza mikakati ya TPDC katika kutatua changamoto ya vituo amesema, Kituo kinachojengwa na TPDC eneo la Chuo Kikuu Dar es salaam ambacho kitakamilika mwezi Desemba, 2024 kitakuwa na pampu nne za kujaza gesi, na kila pampu itakuwa na nozeli mbili hivyo kutakuwa na nozeli nane zenye uwezo wa kujaza CNG kwenye magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku kitajaza zaidi ya magari 2000 na kitakuwa na uwezo wa kushindilia na kujaza gesi (CNG) kwenye malori matatu (CNG tube trailers) kwa wakati mmoja  sawa na malori 24 kwa siku yatakayosafirisha na kusambaza gesi kwenye maeneo mbalimbali.

Aidha, TPDC kwa kushirikiana na Sekta binafsi ipo katika mkakati wa kukamilisha ujenzi wa vituo 13 vya kujaza gesi asilia kwenye magari ifikapo mwezi Julai, 2025.

Katika hatua nyingine Mha. Gilbert amesema kuwa, makampuni mbalimbali yanaendelea kujitokeza kujenga vituo vya gesi ikiwemo kampuni ya Mafuta ya PUMA ambayo itaanza ujenzi wa vituo viwili eneo la Mbezi beach na Tegeta Jijini Dar es salaam.