Waziri wa Maji, Nishati na Madini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Shaib Kaduara apongeza juhudi za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika jitihada za kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.

Waziri Kaduara amesema hayo alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika Kongamano la kumi la jotoardhi Barani Afrika (ARGeo-C10) leo tarehe 25.10.2024 katika Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere JNICC Jijini Dar es salaam.

Kaduara amesema, ‘’naipongeza TPDC kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa Wanachi mbalimbali.”

Akielezea Mjiofizikia Mwandamizi kutoka TPDC Bw. Gaston Canuty amesema lengo la TPDC kushiriki katika Kongamano hilo ni kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

“TPDC kama Shirika la mafuta la Taifa tunaunga mkono juhudi hizo kwa kufanya utafiti wa mafuta na gesi, kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani na nishati safi ya kupikia majumbani,” amesema Canuty.

Aidha, Canuty amesema, utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi unaotekelezwa na TPDC  utatumika kama daraja la kujenga miundombinu ya kuendeleza nishati Jadidifu.