CP AWADHI ATEMBELEA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA SONGOSONGO

Kamishna wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini CP Awadhi Juma  leo tarehe 23/01/2023 amefanya ziara ya kutembelea miundombinu ya gesi asilia iliyopo Songosongo Mkoani Lindi inayosimamiwa na Kampuni Tanzu ya TPDC (GASCO).

Ikiwa lengo la ziara  hiyo ni kujionea hali ya usalama wa miundombinu ya gesi asilia katika maeneo yanayopitiwa na bomba la gesi asilia ambapo Jeshi hilo ni chombo muhimu kinachohusika  na jukumu la kulinda  usalama wa raia na mali zao pamoja na  rasilimali za nchi.

Akizungumza katika ziara hiyo na Makamanda wa Mikoa na Wilaya zinazopitiwa na bomba gesi asilia  CP Awadhi amesema Jeshi la polisi nchini linawajibu wa kuhakikisha rasilimali za nchi zinakuwa salama wakati wote ili nchi iweze kusonga mbele kuchumi.’’Gesi ni moja ya rasilimali muhimu sana kwa nchi yetu hivyo usalama usipoimarishwa katika miundombinu hiyo ya gesi ni dhahiri uchumi na maendeleo ya nchi yatayumba kwani mpaka sasa 60% ya umeme nchini unatokana na gesi asilia.’’

Vilevile, CP Awadhi amewasisitiza kuendelea kuwajibika ipasavyo kwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija,nidhamu na uadilifu hasa kwenye maeneo yanayohitaji ulinzi madhubuti.’’Jeshi la polisi limeingia makubaliano na TPDC ya ulinzi na usalama wa miundombinu  ni nvyema tukaimalisha ulinzi wa miundombinu hiyo na kufanya doria za mara kwa mara pamoja na kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya miundombinu.’’

Nae Mkuu wa Kitengo cha Usalama GASCO Bw.Fred Mfikwa alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa ushirikiano na amesema TPDC imekua ikishirikiana kwa karibu na Makamanda wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha ulinzi wa miundombinu ya gesi asilia toka Mtwara mpaka DSM inakua salama.

Bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es salaam lina urefu wa kilometa 551 na limepita katika vijiji  139.