Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo mama cha kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG Mother Station) kinachojengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo ameeleza kwamba kukamilika kwa Kituo hicho mapema mwaka huu kutawawezesha Watanzania wengi, hususan wanaotumia gesi asilia kwenye magari kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 09 Januari, 2025 Jijini Dar es salaam baada ya kukagua Kituo hicho Dkt. Biteko amesema kwamba, kuanzia Februari 3 mwaka huu, Kituo kitaanza rasmi kutoa huduma ya kujaza gesi asilia kwenye magari.
Aidha, Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali imeelekeza kujengwa kwa vituo vingine vya gesi asilia, ambapo vituo saba vya ziada vinajengwa na Sekta binafsi katika Mkoa wa Dar es Salaam huku akiongeza kuwa Serikali imepanga kuanzisha vituo vinavyotembea (CNG Mobile Station) vya kujaza gesi asilia katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kwamba wamekubaliana na Shirika la Mabasi yaendayo Haraka (DART) kuleta mabasi yanayotumia gesi asilia, hatua hii inalenga kuhamasisha Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kimetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo,Profesa William Anangisye amefafanua kuwa mradi huo utatoa fursa kwa Wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi kutumia Kituo hicho kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.Vilevile Kituo hicho kitakapokamilika kitatoa fursa za ajira kwa Watanzania.
Aidha, gharama za ujenzi wa mradi wa Kituo mama cha CNG ni kiasi cha shilingi Bilioni 14.5 hadi kukamilika kwake.
Halikadhalika, huduma zitakazotolewa katika Kituo cha CNG ni pamoja na huduma ya kujaza CNG kwenye magari yote (malori, mabasi, gari ndogo za abiria na pikipiki za miguu mitatu/bajaji), Kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari 8 kwa wakati mmoja na kwa siku kikitoa huduma kwa magari 1,200 pia Kituo kitakuwa na dedicated pumps kwaajili ya kujaza malori matatu ya kupeleka gesi kwenye vituo vidogo na viwandani.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment