Kagera ipo Imara Kulinda Bomba la Mafuta 


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge alisema,  Mkoa huo  umejipanga kuulinda mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima,  Uganda hadi Chongoleani Mkoani Tanga.

Meja Jenerali Mbuge amesema hayo wakati wa  mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mkoani Kagera,  ambapo  amezungumzia ujio wa mradi wa bomba hilo nchini ukitokea Uganda.

Alisema Mkoa wa Kagera hauna viwanda vingi,  hivyo  ujio wa mradi huo wa bomba la mafuta ghafi  linalopita Mkoani humo utaleta chachu ya kukua kwa uchumi wa Mkoa na maendeleo ya wananchi wake.

“Niwahamasishe wananchi wa Tanzania hasa wa Mkoa wa Kagera kuchangamkia fursa za mradi huu ambao umekuja muda muafaka na Serikali inausimamia kwa ukaribu sana,  ili kuleta faida kwa Taifa,” alisema Meja Jenerali Mbuge.

Huu ni mradi wa Kimkakati wa Serikali na unatekelezwa na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na  unatarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

 Aidha, Mradi huu unatekelezwa kwa kiasi cha fedha Dola  Bilioni 5.1 za Kimarekani ambazo ni sawa na shilingi takribani trilioni 11 zinatarajiwa kutumika  hadi kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo wa  bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.