Nchi Bado Haijagundua Mafuta, Tpdc Inaendelea Na Utafiti Eyasi


Simiyu.
Waziri wa Nishati Mhe. January Yusuf Makamba alisema Tanzania bado haijagundua
mafuta, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea na
jitihada za utafiti katika Bonde la Eyasi Wembere.
Mhe. Makamba aliyasema hayo alipokuwa akifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu pamoja na Waandishi wa Habari, tarehe 13 Julai, 2022 Mkoani Simiyu.
“Nchi yetu bado haijagundua mafuta, kumekuwa na jitihada za makusudi
zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Shirika la TPDC ili kuhakikisha na
sisi tunagundua mafuta. Kwa sasa TPDC ipo katika hatua nzuri ya utafiti wa mafuta
katika Bonde la Eyasi Wembere. Kutokana na matokeo ya kitaalamu, yapo matumaini
makubwa kwamba huenda mafuta yakagunduliwa,’’alisema Makamba.
Mheshimiwa Makamba aliongeza, “Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya Kimkakati
inayotekelezwa na Serikali na unahusisha Mikoa mitano (5) ambayo ni; Arusha (Wilaya
ya Karatu), Singida (Wilaya za Iramba na Mkalama), Simiyu (Wilaya ya Meatu),
Shinyanga (Wilaya ya Kishapu) pamoja na Tabora (Wilaya ya Igunga).”
Aidha, Meneja wa Mradi wa utafutaji mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere kutoka
TPDC, ndugu Sindi Maduhu, alisema, tangu kuanza kwa mradi 2015, kuna baadhi ya
hatua ambazo mradi umepitia,hatua hizo zilihusisha shughuli za kisayansi kama vile
ukusanyaji wa taarifa za usumaku na uvutano kwa kutumia ndege, kuchoronga
mashimo mafupi ya utambuzi wa miamba na kwa sasa Shirika linaendelea na shughuli
ya ukusanyaji wa taarifa za kijiokemia zitakazowezesha kutambua uwezekano wa
uwepo wa mafuta yanayovuja kutoka ardhini, kwa kutumia teknolojia maalumu ya
moduli (Amplified Geochemical Imaging).”
Maduhu aliongeza kuwa, “hatua hizi za kisayansi zinatoa matumaini makubwa ya
uwepo wa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere. Hii inatokana na sababu kwamba,
taswira za miamba iliyopo Eyasi Wembere inafanana kwa kiasi kikubwa na taswira za
miamba ya Ziwa Albert nchini Uganda na Ziwa Turkana nchini Kenya, ambapo tayari

mafuta yamegundulika katika sehemu hizo. Hivyo hata sisi tunapoendelea na utafiti
tunaamini huenda tukagundua mafuta ambayo yataleta tija katika uchumi wa Taifa.”
Kitalu cha Eyasi Wembere kipo Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania ndani ya Bonde la
ufa la Afrika Mashariki. Bonde hili linapita katika Mikoa ya Arusha, Singida, Tabora,
Shinyanga na Simiyu. Bonde hili ni moja ya maeneo yenye miamba tabaka yenye
uwezo wa kuhifadhi mafuta au gesi asilia. Aidha, eneo hili lipo katika ukanda mmoja na
mabonde ya Lokichar (Kenya) na Ziwa Albert (Uganda) ambapo mafuta yamegundulika.