Mkurugenzi Mtendaji Wa TPDC Atembelea Maonesho Ya Sabasaba

Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio tarehe 07/07/2022 alitembelea Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) katika banda la TPDC Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika banda hilo Dkt. Mataragio alisema kuwa kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa mpaka sasa ni futi za ujazo Trilioni 57.54 tcf. ‘’Kiasi hiki cha gesi asilia kimeendelea kuwa msaada mkubwa kwa Watanzania kutokana na matumizi yake kufikia asilimia 62 huku kiasi kikubwa cha gesi kikiwa baharini’’.  

Alisema kiasi kikubwa cha gesi ambacho kipo baharini kinatarajiwa kuvunwa kupitia mtambo wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unaotarajiwa kujengwa eneo la Likon’go Mkoani Lindi ambapo gesi itakayopatikana itasafirishwa kwenda kuuzwa kwenye masoko ya nje ya nchi na nyingine kubaki nchini kwa ajili ya soko la ndani. 

Aidha, Dkt.  Mataragio aliwaomba Watanzania kutumia fursa hiyo kwa kuanzisha Makampuni yanayotumia gesi asilia ili waweze kunufaika zaidi na fursa hiyo, pia kwa kutumia gesi asilia watakuwa wameshiriki kuokoa uharibifu wa mazingira.