Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Andrea Motzfeldt Kravik, ameonesha kuridhishwa kwake na maendeleo ya maandalizi ya mradi wa Kimkakati wa Kusindika gesi asilia (LNG) unaotarajiwa kutekelezwa katika eneo la Likong’o Mkoani Lindi, Kusini mwa Tanzania.
Akiwa katika ziara yake Mkoani humo, Mhe. Kravik alitembelea eneo la mradi pamoja na kukutana na Viongozi wa Serikali, Wataalamu wa sekta ya nishati, na wadau mbalimbali wa maendeleo. Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Norway kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, hasa katika sekta ya nishati safi na mazingira.
“Tanzania imepiga hatua kubwa kuelekea kwenye mradi huu. Baada ya kutembelea na kupewa maelezo kuhusu eneo la mradi, mimi pamoja na ujumbe wangu tumefurahi na kuridhishwa na hatua hizi. Vilevile ninaweza kuahidi kwa kujiamini kwamba tumejidhatiti kikamilifu kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mradi huu mkubwa hapa Tanzania,” alisema Mhe. Kravik.
“Mradi wa LNG ni muhimu kwetu sote na nchi ya Norway inajivunia kuwa mshirika wa Tanzania katika kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za gesi asilia zinaleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.”
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amemuhakikishia Mhe. Kravik na ujumbe wake kwamba, Serikali ya Tanzania, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na jitihada za kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji, ikiwemo uwekezaji mkubwa wa mradi wa LNG Mkoani Lindi. Aidha, Mhe. Telaki alielezea umuhimu wa mradi huu hasa katika kipindi hiki ambacho mwelekeo wa Dunia ni kwenye matumizi ya nishati safi, na kwa upekee kabisa, mradi huu utachochea ukuaji wa sekta nishati, viwanda na kilimo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji, Uzalishaji na Uendelezaji kutoka TPDC Bw. Paschal Njiko ameelezea umuhimu wa mradi huo na hatua iliyofikiwa hadi hivi sasa, “Tayari TPDC imekamilisha hatua ya utwaaji wa ardhi yenye ukubwa wa hekari 2071 kwa kulipa fidia Wananchi husika. Eneo hili la mradi linahusisha mitaa mitatu ya Kata ya Mbanja ambayo ni Likong’o, Mto Mkavu na Masasi ya Leo kutoka Manispaa ya Lindi. Hatua inayosubiriwa sasa ni kukamilika kwa majadiliano baina ya Serikali na Wabia wa mradi ambayo ni makampuni ya nishati ya Kimataifa, Shell na Equinor,” alisema Bw. Njiko.
Njiko aliongeza kuwa kwa upande wa TPDC itakuwa ni fursa kubwa kufanya shughuli za kibiashara za kuzalisha na kuuza LNG sambamba na kuongeza upatikanaji wa gesi ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Mradi wa LNG, unakadiriwa kuwa na thamani ya dola Bilioni 42 sawa na Trilioni 90 za Kitanzania, unatarajiwa kuwa moja ya miradi mikubwa zaidi ya nishati Afrika Mashariki na Kati. Mradi huu unahusisha ushirikiano wa Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za kimataifa za nishati za Shell na Equinor.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment