Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji katika tafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini ili Watanzania wanufaike na rasilimali zilizopo.
Dkt.Biteko ameyasema hayo leo tarehe 10.09.2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya leseni ya uendelezaji eneo la ugunduzi wa gesi kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na ARA Petroleum katika kisima cha Ruvuma Ntorya mkoani Mtwara.
“Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt.Biteko.
Ameongeza kuwa, jitihada za Serikali zinaenda sambamba na kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili liweze kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa thamani wa mafuta na gesi.
Aidha, ametoa wito kwa TPDC na Kampuni ya ARA Petroleum kutoa kipaumbele kwa wazawa katika utoaji wa ajira ili kuwe na muunganiko kati ya Wananchi na ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo.
Naye,Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kirumbe Ng’enda amesema utoaji wa leseni ya uendelezaji Kitalu cha gesi cha Ruvuma ni hatua kubwa ya maendeleo nchini.
“Kitalu hiki kitazalisha futi za ujazo trilioni 1.6, hili ni jambo kubwa sana na la kuipongeza Serikali, tunampongeza Rais Dkt. Samia ambaye yeye ndie jemedari wa mapambano ya kuleta maendeleo nchini,” amesema Mhe. Ng’enda.
Vilevile, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba, amesema Tanzania ina historia ndefu katika matumizi ya gesi asilia kuanzia miaka ya sabini baada ya ugunduzi wa gesi asilia katika Kisiwa cha Songosongo.
‘’Ugunduzi wa gesi asilia nchini umefungua mlango endelevu wa uhifadhi wa mazingira na kuimarika kwa usalama wa nishati,’’ amesema Mha. Mramba.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment