Serikali imeridhia ombi la kuondoa ushuru wa shilingi 382 iliyokuwa imepanga kuweka kwenye kila kilo ya gesi asilia inayotumika kwenye magari kuanzia mwaka ujao wa fedha 2024/25.

Ushuru huo umeondolewa kufuatia ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambayo imeeleza kuwa haikubaliani na ushuru huo kwani sekta ya gesi bado ni changa na inaendelea kukua taratibu na hadi sasa haijaweza kutumika kikamilifu nchini kutokana na gharama za kufunga mfumo wa kutumia gesi pamoja na uhaba wa vituo vya kujazia gesi.

Wabunge wengi waliochangia hotuba ya Bajeti ya Serikali 2024/25 walipinga kuanzishwa kwa ushuru huo wakisema kuwa unaenda kinyume na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuchagiza matumizi ya nishati safi nchini.

Aidha, kamati imeshauri Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumika kuunganisha mfumo wa gesi ili kupunguza gharama za kusimika mfumo huu kwenye magari ambazo kwa sasa gharama za ufungaji zinakadiriwa kuwa kati ya shilingi milioni 2 hadi milioni 3, kiwango ambacho ni kikubwa.