TPDC Imetoa Jumla ya Shilingi 1.5 Bilioni kwenye Shughuli za Kijamii Nchini
Hayo yamezungumzwa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Usalama cha GASCO kutoka Kampuni Tanzu ya TPDC ndugu Fred Mfikwa wakati akikabidhi viti na meza 85 kwa Shule ya Sekondari ya Kikanda Mkoani Lindi.
“Uwajibikaji kwa jamii ni kipaumbele cha Shirika ikiwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kuinua huduma za kijamii kwenye maeneo ambayo miradi ya gesi asilia inatekelezwa”, ameeleza ndugu Mfikwa.
Mfikwa amebainisha kuwa, kwa kiasi kikubwa Shirika limekuwa likichangia katika nyanja kuu nne ambazo ni sekta ya afya, maji, elimu pamoja na utawala bora, hayo ni maeneo ambayo yanagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi
Ndugu Mfikwa amongeza kuwa kwa upande wa Mkoa wa Lindi TPDC imetekeleza ujenzi wa miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji katika Kijiji cha Songosongo na Kilangala B, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule, ujenzi wa madarasa, ujenzi wa maabara shuleni, kudhamini michezo pamoja na ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali za Mitaa na Vijiji.
Aidha kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bi. Kwigema Anthony akiongea katika hafla ya kukabidhi samani hizo amesema kuwa kilichofanyika ni muendelezo wa jitihada za TPDC katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya, maji, utawala bora na hili la elimu nchini.
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa samani baadhi ya Walimu, Viongozi wa Kata na Wanafunzi wameishukuru TPDC kwa kuwapatia samani na kueleza kuwa samani hizo zitawasaidia wanafunzi kujifunza kwa ufanisi mkubwa na vitapunguza changamoto ya viti na meza ambayo ilikuwepo hapo awali.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekuwa likitekeleza Sera ya Shirika ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ya mwaka 2017, lengo likiwa ni kuendelea kudumisha uhusiano kati ya Shirika na jamii zinazoguswa na miradi ya mafuta na gesi asilia pamoja na maendeo mengine nchini.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment