Tpdc Kujenga Bomba La Gesi Jipya Mtwara 


Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza mchakato wa Ujenzi wa

Bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 35.

Mchakato huo umeanza kwa  kufanya mkutano wa uhamasishaji kwa wananchi wa

Kata ya Madimba, Moma, Mbawala na Nanguruwe kuhusu ujenzi wa

mradi huo ambao utaanzia Kijiji cha Ntorya.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dustan Kyobya

amesema hatua ya awali ya utafiti wa mkuza utakaotumika kupitisha bomba

ulishafanyika awali na kubaini vijiji 12 vitakavyopitiwa na bomba.

Vijiji hivyo ni Namayakata, Ngorongoro, Mbawala, Mwindi, Nachenjele, Maili kumi,

Ding’ida, Likweta, Minyembe, Namidondi na Mendachi.

Mhe. Kyobya amesema hatua inayokwenda kufanyika sasa ni zoezi la uthamini wa mali

kwenye mkuza wa bomba wenye upana wa mita 20.

Lengo la zoezi hilo ni kutambua maendelezo yaliyofanyika katika ardhi hiyo ikiwemo

nyumba, mazao na mali zingine  ili kubaini thamani yake na kuandaa taratibu za malipo

ya fidia kwa wamiliki watakaopisha mradi huo.

Aidha Kyobya amewataka wananchi wa maeneo ya yanayopitiwa na mkuza wa bomba

kutoa ushirikiano kwa TPDC wakati watakapopita kwenye maeneo yao katika zoezi

uthamini.

”Naomba wananchi muwe wakweli  kutoa taarifa sahihi za mmiliki wa eneo na

pia muwape ushirikiano wataalamu watakaopita kwenye maeneo yenu wakati wa  zoezi

hilo kuepusha migogoro mbalimbali ya ardhi.’’

Halikadhalika, Mha. Emmanuel Gilbert kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania

(TPDC) amesema utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa nishati ya

gesi asilia kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa

umeme, matumizi ya gesi kwenye magari, matumizi viwandani na majumbani.