Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio alisema, ‘’kufikia mwezi Machi, 2023 Shirika litakuwa limekamilisha ujenzi wa vituo vinne vya kujaza gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) na kuanza kufanya kazi kwa ajili ya magari na majumbani.’’
Hayo yalibainishwa Juni 8, 2022 wakati wa utiaji saini wa makubaliano kati ya TPDC na Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ya kutumia eneo kujenga miundombinu ya kuzalisha gesi iliyoshindiliwa (CNG) kwa ajili ya kujaza kwenye magari na kuwezesha kusafirisha gesi hiyo katika Mikoa ambayo haina miundombinu.
Kati ya vituo hivyo kituo kikubwa kitajengwa eneo la Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kikitazama barabara ya Sam Nujoma jirani na hosteli za Magufuli. Kituo hiki kitakuwa kikizalisha gesi iliyoshindiliwa kwa ajili ya kujaza katika magari na kuhudumia vituo dada vitatu.
Vituo dada vitakavyohudumiwa na kituo hicho vitajengwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, eneo la Kiwanda cha Kairuki na kituo cha tatu kitajengwa katika eneo la Soko Kuu la Samaki la Feri.
Dkt. Mataragio alisema, kujengwa kwa vituo hivyo kumelenga kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati ya gesi asilia hasa kwa maeneo ambayo kwa sasa hayajafikiwa na miundombinu ya usambazaji wa gesi kwa njia ya mabomba .
Mradi huu uliasisiwa katika mwaka wa fedha 2018/19 na ilipofika mwaka 2020, TPDC ilikamilisha usanifu wa mradi kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo na kuviingiza katika mpango wa kutafuta wakandarasi wa ujenzi katika mwaka wa 2022-2023.
Aidha, katika ujenzi huo, baadhi ya gesi asilia itakayozalishwa eneo la UDSM itasafirishwa kwa magari maalumu kwenda kwenye vituo dada ambavyo vitajengwa sehemu ambazo kwa sasa hazina mabomba ya kusambaza nishati hiyo.
‘’Kituo cha CNG katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuanzia kitatumika kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kuzalisha mvuke (steam) ya kufulia pamoja na kupikia katika hospitali hiyo na baadaye kitaanza kusambaza gesi kwa wateja mbalimbali wa majumbani na Taasisi.
- By:admin
- 0 comment