Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefanya kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi kwa lengo la kutathimini mambo yaliyofanyika katika Shirika ili kuzidi kuboresha ufanisi wa kazi

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 18/02/2025 katika ukumbi wa mikutano wa Morena Mjini Morogoro na kufunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC Mhe. Balozi Ombeni Sefue.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mhe. Balozi Sefue   ameeleza kuwa kupitia baraza hilo la wawakilishi wa wafanyakazi linatoa fursa muhimu ya Wafanyakazi na Menejimenti kufanya  tathimini  ya kina  ya miaka mitatu ya utendaji kazi wa  Shirika  na kuona kama limeweza kufanikiwa  kufikia malengo na mipango iliyowekwa katika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa gesi na kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi kwaajili ya matumizi mbalimbali.Aidha alieleza kuwa tathmini hiyo inatoa fursa ya kujipanga upya kwa miaka mingine ijayo ambapo TPDC itatoa mchango mkubwa sana katika kufikia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.

 ‘‘Malengo ya TPDC yakifanikiwa kama yalivyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Shirika, naiona   TPDC ikiwa na mchango mkubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050,’’ amesema Balozi Sefue.

Vilevile, Balozi Sefue amewasisitiza Watumishi na Menejimenti ya TPDC kudumisha umoja, ushirikiano na weledi katika utendaji wa kazi za Shirika ili kuleta matokeo yenye tija kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

‘’Wafanyakazi ndio watekelezaji wakuu wa mipango ya Shirika, wanapaswa kupewa ushirikiano na kujengewa umoja katika utendaji wa kazi zao,’’amesisitiza Balozi Sefue.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi TPDC Bw. Ridhiwani Manzi amesema kuwa Baraza hilo la Wafanyakazi lina umuhimu mkubwa kwa Shirika, Wafanyakazi na Menejimenti ili kuweza kupanga mikakati ya maendeleo ya jumla kwa Shirika zima pamoja na maendeleo ya Wafanyakazi katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi. 

“Baraza hili limekuwa kiungo kikubwa sana kwa Wafanyakazi na menejimenti katika kusimamia pamoja muendelezo wa mipango ya Shirika letu pamoja na kuboresha maslahi ya Wafanyakazi na Shirika,” amesema Manzi.