Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Rosetta ya nchini Misri wamesaini mkataba wa awali wa ubia wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi asilia kwa mfumo wa Mini LNG.

Mkataba huo umesainiwa leo tarehe 17/05/2024 katika ukumbi wa mikutano wa TPDC ulioko Jengo la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile amesema mradi wa usambazaji wa gesi asilia kwa kutumia Mini LNG utasaidia kupanua wingo wa usambazaji wa gesi asilia na kuwezesha matumizi yake nchi nzima. “hatua hii ya utiaji saini inaonyesha juhudi za dhati za Serikali kupitia TPDC katika kuhamasisha usambazaji wa gesi asilia nchini kote, lengo ambalo sote tunaweka bidii ili liweze kutimia’’.

Aidha,Dkt. Andilile amebainisha kuwa mahitaji ya gesi asilia nchini ni makubwa ambapo hadi sasa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, na Dar es Salaam pekee ndio imefikiwa na mtandao wa gesi asilia hivyo kuna uhitaji wa gesi asilia kwa mikoa mingine hali inayoonyesha ni kwa kiasi gani soko la gesi asilia ndani ya nchi ni kubwa na uwekezaji zaidi unahitajika ili kuweza kukaribia mahitaji ya watumiaji wa gesi viwandani, majumbani na kwenye magari.

Nae,Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPDC  Bw. Paul Makanza amesema  mradi wa Mini LNG sio tu utakuza viwanda pia utaleta  manufaa ya kiuchumi kwa jamii kwa kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na kuongeza matumizi ya gesi asilia viwandani jambo ambalo litachangia ukuaji na ustawi wa taifa letu.

Halikadhalika, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ndugu Mussa Makame amesema gharama za uwekezaji wa mradi wa usambazaji wa gesi asilia Mini LNG ni Dola milioni 100.

Ndugu Makame amesema, mradi huo ambao ni sehemu muhimu ya mkakati mpya wa TPDC, utatekelezwa kupitia mpango wa Ubia kati ya TPDC, Rosetta na Africa 50, ambapo TPDC atamiliki hisa 30% Kampuni ya Rosetta 44% na Kampuni ya Afrika 50 (26%) hatua hii ya kimkakati inasukuma sekta ya nishati nchini Tanzania kuelekea mustakabali endelevu.

Akibainisha mikoa itakayoanza kunufaika mara baada ya kukamilika kwa mradi Makame ameitaja kuwa ni Morogoro, Dodoma, Mwanza, Shinyanga, Iringa, Mbeya na Tanga ambayo pia itajengewa mabomba ya kuwezesha usambazaji wa gesi hiyo ili kuongeza wigo wa matumizi ya gesi asilia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rosetta Karim Shaaban ameishukuru Serikali na taasisi zake kwa kuwezesha kufikia makubaliano ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia nchini. “ mradi huo wa kusambaza gesi  utatusaidia sisi Wawekezaji  kuchagia  pato la Tanzania,’’ amesema Karim.