Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania limefanya Bonanza la ujirani mwema katika Kata ya Mnazi Mmoja iliyopo Mkoani Lindi ambayo inapitiwa na miundombinu ya bomba la gesi asilia.
Bomba la kusafirisha gesi asilia mkoani Lindi limepita katika Vijiji/Mitaa kadhaa ambayo wananchi wake wanahusika kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo.
Bonanza hilo la michezo lililoandaliwa na TPDC lilizishindanisha timu nne za mpira wa miguu kutoka Kata ya Mnazi Mmoja mbazo ni timu ya Mnazi Mmoja, timu ya Veteran, timu ya Oik Academy pamoja na timu ya Texaz.
Akizungumza wakati wa mchezo wa fainali kati ya Mnazi Mmoja na Veteran Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga alisema TPDC Bonanza ni muhimu kufanyika kwa kuwa TPDC kwa niaba ya Serikali inazitangaza kwa Wananchi kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali ikiwemo mradi wa LNG (kubadili gesi asilia kuwa kimiminika) unaotekelezwa eneo la Likongo Mkoa wa Lindi pamoja na mradi wa kusambaza gesi asilia katika Kata ya Mnazi Mmoja.
‘’Tunategemea katika miezi michache ijayo nyumba 209 za Kata ya Mnazi Mmoja zitaunganishiwa na gesi asilia kwaajili ya matumizi ya kupikia lengo ikiwa ni kuwahamasisha Wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa,’’ alisema Mhe. Shaibu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka TPDC Bi. Marie Msellemu alisema lengo la TPDC Bonanza ni kuendelea kujenga na kukuza uhusiano kati ya TPDC na Wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mkuza wa bomba katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam.
Aidha, ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Bonanza hilo lilienda sambamba na zoezi la upimaji afya bure na kwa hiyari kwa Wananchi wa Kata ya Mnazi Mmoja.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment