Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa mradi wa utafiti wa mafuta na gesi kwenye Bonde la Eyasi Wembere lililopo katika mikoa ya Simiyu, Singida na Arusha,Tabora na Shinyanga utekelezaji wake umefikia asilimia 40.
Hayo yameelezwa na Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC walipotembelea eneo la mradi wa utafiti wa mafuta na gesi katia Bonde la Eyasi Wembere na kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Shirika hilo.
‘’Tumejionea kazi nzuri ya utafiti wa mafuta na gesi asilia, na tunaipongeza Menejimenti ya TPDC kwa kusimamia vyema utekelezaji wa utafiti wa mafuta katika Bonde hili kwani hatua iliyofikiwa sasa inaridhisha, pia tunaishukuru Wizara ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt.Doto Biteko kwa kuendelea kuunga mkono na kusimamia vizuri shughuli za Bodi,’’ alisema Balozi Kalaghe ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za Serikali shilingi Bilioni 43 ulianza mwaka 2015 ambapo shughuli zinazoendelea kufanyika ni uchukuaji wa taarifa (Data) za mitetemo na kuzichakata ili kupata uhakika wa uwepo wa mafuta au gesi.
Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC kwenye ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji Bw.Derick Moshi alieleza kuwa mradi wa Eyasi Wembere ni wa kimkakati katika nchi na jukumu la TPDC ni kusimamia shughuli zikamilike kwa wakati.
Naye, Kaimu Meneja wa Utafutaji kutoka TPDC Bw. Simoni Nyalusi alisema kuwa shughuli za utafiti zinazofanyika katika Bonde hilo, zinatekelezwa kwenye maeneo mawili ambayo ni eneo la nchi kavu na eneo la majini ndani ya Ziwa Eyasi.
Alisema kuwa katika eneo la nchi kavu wamefanikiwa kufikia asilimia 40 ya utafiti huo, ambapo alibainisha kuanza kuonekana kwa viashiria mbalimbali ambavyo vimetoa matumaini makubwa ya uwepo wa mafuta na gesi.
Aidha, Wananchi wanaoishi kwenye Vijiji vinavyoguswa na shughuli za utafiti kwenye mikoa iliyopitiwa na mradi wamekua na matumaini ya matokeo chanya ya mradi huo kwani tayari wameanza kuona faida za moja kwa moja ikiwemo kupata fursa za ajira
Mkazi wa Kijiji cha Nyahaa Kitongoji cha Ulianzobhe Wilaya ya Mkalama Bw.Njibu Tinha, alieleza kuwa, vijana wengi wamepata ajira kwenye shughuli za mradi ikiwemo ulinzi, mafundi umeme, udereva pamoja na shughuli za ujenzi.
‘’Kwetu ni faraja kubwa sisi kama Wanachi tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Wataalamu wanaohusika na mradi ili shughuli za utafiti zisikwame,’’ alisema Njibu.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment