TPDC Yatunukiwa Tuzo
Dar es salaam,
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio alipokea tuzo ya heshima kutoka kwa Serikali ya Uganda kupitia Mamlaka ya Uwekezaji nchini humo (Uganda Investment Authority-UIA) kwa kutambua mchango wake wa kitaalam katika kufanikisha mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) pamoja na kufikia maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (FID) ya mradi.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa tarehe 30 Juni, 2022 Jijini Dar es salaam kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. Mataragio na Ndugu Bryan Mbwana ambaye ni mwakilishi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji nchini Uganda.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Dkt. Mataragio alisema, TPDC kwa niaba ya Serikali wamekuwa ni washiriki wakubwa na wabia katika mradi wa EACOP ambapo wamefanya jitihada mbalimbali za kuwezesha mradi kufikia maamuzi ya mwisho ya uwekezaji (Final Investment Decision) yaliyofanyika mwishoni mwa mwezi Februari, 2022 chini Uganda.
Pia, Dkt. Mataragio alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Mamlaka ya Uwekezaji nchini Uganda (UIA) kwa kutambua mchango wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika ushiriki wa mradi wa EACOP.
‘’Natoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Uganda kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Uganda kwa kutambua mchango wa Serikali, Wizara ya Nishati, TPDC, Wadau mbalimbali wa Sekta ya Nishati pamoja na Waandishi wa Habari katika ushiriki wa matukio mbalimbali ya mradi huu wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga-Tanzania.
Aidha, Dkt. Mataragio aliendelea kusema tuzo waliyopewa ni ya Watanzania wote kwani kwa namna moja au nyingine wameshiriki katika matukio mbalimbali yaliyochangia kufanikisha mradi huo.
Naye, mwakilishi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Uganda Ndugu Bryan Bwana alisema, Mamlaka ya Uwekezaji nchini Uganda imeamua kuipatia tuzo TPDC kama ishara ya kutambua mchango mkubwa uliofanywa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia TPDC.
Bwana aliongeza kwa kusema kuwa miongoni mwa faida wanazopata ni fursa ya ajira zaidi ya 10,000 zilizopatikana kwa wananchi wao ikiwemo ajira 1000 za utaalamu ambapo wataalam wanaendelea na kazi hadi hivi sasa.
‘’Mamlaka ya Uwekezaji nchini Uganda pamoja na Sekta ya mafuta na gesi tunasema asante sana kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na TPDC, tuzo hii ni ishara ya upendo kutoka Sekta ya mafuta na gesi ya Uganda.
Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga unahusisha bomba lenye urefu wa Kilometa 1443.Gharama za mradi huu zinakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani Bilioni 5.1. Mradi huu umepita katika Mikoa nane (8) ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma,Manyara na Tanga. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa wanahisa wanne ambao ni Kampuni ya Taifa ya mafuta ya Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya TOTAL ya Ufaransa pamoja na Kampuni ya CNOOC ya China.
- By:admin
- 0 comment