Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaounganisha bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, umefikia asilimia 45.5 katika hatua ya ujenzi ambapo shughuli za ujenzi zinaendelea katika maeneo mbalimbali kuanzia Mtukula Kagera mpaka Chongoleani Tanga.

Taarifa hii imetolewa Oktoba 18, 2024, na Mratibu wa Mradi wa EACOP kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Asiadi Mrutu, wakati Wajumbe wa Tume ya Kitaifa ya Mipango ikiwa imeambatana na Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC na Menejimenti ya TPDC ilipotembelea eneo la ujenzi wa Kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto kwenye mabomba katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega, mkoani Tabora.

Mrutu amesema kufuatia jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utekelezaji wa mradi huu kwa ujumla umefikia asilimia 45.5 ambapo shughuli za ujenzi zinaendelea katika maeneo mbalimbali kuanzia Mtukula Kagera mpaka Chongoleani Tanga na kwamba mpaka kufikia Oktoba 2024 Serikali kupitia TPDC imechangia mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 977.6 kwenda kwenye Kampuni ya Mradi EACOP.

“Kiwanda hiki kinaendelea na uzalishaji wa mabomba ambapo mpaka sasa jumla ya mabomba yenye urefu wa kilomita 70.7 yamewekwa mifumo ya kupasha na kutunza joto. Ujenzi wa bomba na miundombinu yake unaendelea,”amesema Mrutu.

Mpaka sasa mradi umeleta mafanikio makubwa ikiwemo fursa za ajira 7,584, manunuzi ya huduma na bidhaa za ndani ya nchi zenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 833.7, mapato kwa Serikali takribani Shilingi Bilioni 40, uhaulishaji wa teknolojia toka kwa Wakandarasi,” ameeleza Mrutu.

Ameeleza kuwa ujenzi wa Kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto kwenye mabomba uliopo Kijiji cha Sojo Wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora umefikia asilimia 93 na ulizinduliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko mnamo Machi 26, 2024.

“Pamoja na kuwa mwanahisa, TPDC inamiliki ardhi ya mkuza wa bomba na maeneo ya ujenzi wa makambi ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kulipa fidia jumla ya shilingi Bilioni 35.1 kwa Wananchi 9,858 kati ya 9,927 sawa na 99.3%. Vilevile mradi umefanikiwa kujenga nyumba 340 za makazi mbadala kwa Wananchi 294 waliopoteza makazi kwenye maeneo ya mradi. Serikali inaendelea kushirikiana na Wanahisa wengine ili kuhakikisha fedha za mradi zinapatikana kwa wakati na utekelezaji unaendelea ili kufikia malengo. Ujenzi unatarajia kukamilika katikati mwa mwaka 2026,” ameongeza Mrutu.