Ujenzi wa Karakana ya Kupaka Rangi Mabomba Eneo la  Sojo Unaendelea 


Shughuli za ujenzi wa Karakana ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika Kijiji cha Sojo, Nzega Mkoani Tabora uko katika hatua nzuri.

Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kinachoendelea sasa ni wakandarasi kutoka kampuni nne tofauti wanashirikiana  kujenga kiwanda kitakachotumika kuandaa mabomba na kuyaongezea uwezo wa kutunza joto pamoja kupaka rangi.

Akizungumza katika eneo la mradi kinapojengwa kiwanda hicho ambapo ni kilomita 701 kutoka Hoima nchini Uganda unapoanzia mradi huo, Mratibu wa Mradi Taifa kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw.Asiad Mrutu amesema, eneo hilo litakuwa likipokea vipande vyote vya mabomba zaidi ya  86,000 yatakayotumika katika ujenzi huo.

Mrutu amesema, mradi huo utakapokamilika utakuwa msaada mkubwa kwa Taifa hasa katika kuchochea Uchumi pamoja na maendeleo ya Watanzania.

Amesema wakati shughuli za ujenzi zikiendelea wakazi 37 ambao wamehamishwa kupisha eneo hilo wamejengewa nyumba pamoja na kupatiwa mafunzo ya kilimo na ujasiliamali ili kukuza vipato vyao.

Aidha, kutokana na umuhimu wa mradi huo ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kufanikisha mradi kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki umepita katika Mikoa 8 ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Mradi huu utagharimu kiasi cha fedha takribani shilingi trilioni 11 hadi kukamilika kwake na  utazalisha ajira zaidi ya elfu kumi na fursa nyingine za kiuchumi kwa Taifa.