Ujenzi wa Kituo Mama cha Kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG Mother Station) kinachojengwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) eneo la Chuo Kikuu Dar es salaam umefikia asilima 80 hadi kukamilika kwake na imeelezwa kuwa mwishoni mwa mwezi Januari,2025 Kituo hicho kitaanza kutumika kusambaza nishati hiyo muhimu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 06 Januari, 2025 Jijini Dar es salaam, baada ya kukagua Kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio amesema awali Serikali iliahidi kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo mnamo mwezi Desemba,2024 lakini umechelewa baada ya meli iliyokuwa imebeba mitambo hiyo kutoka China kuchelewa kufika nchini.

Akieleza hatua ya ujenzi wa Kituo hicho Dkt. Mataragio amesema mitambo imeshasimikwa na kinachoendelea kwa sasa ni kazi ndogogondogo za kuunganisha mfumo wa umeme ili kuanza kufanya kazi.

Aidha, amesema hadi kufikia Januari 16, 2025 ujenzi utakuwa umekamilika na kuanza majaribio huku akiwahakikishia watumiaji wa nishati hiyo kuanza kupata huduma kituoni hapo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu.

Naye Meneja Mradi wa CNG- TPDC Mhandisi Aristedes Katto amesema kukamilika kwa Kituo cha CNG kutasaidia gesi asilia kufika maeneo mbalimbali ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya mabomba ya gesi. ‘’Mradi huu utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya gesi asilia wa Wananchi wanaotumia gesi asilia kwenye magari yao badala ya petroli na diseli.’’

Ujenzi wa mradi wa Kituo mama cha CNG hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.5 kikijumuisha ununuzi wa magari tisa na ujenzi wa vituo viwili vya kujazia gesi kwenye magari katika maeneo ya Muhimbili Dar es salaam na Kibaha mkoani Pwani.