VITUO 9 VYA KUJAZA GESI ASILIA KWENYE MAGARI KUJENGWA

Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. Wellington Hudson amesema jumla ya vituo tisa (9) vya kujaza gesi asilia kwenye magari vinatarajia kujegwa na kukamilika katika kipindi cha miezi 24.
Dkt. Hudson ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam wakati akifanya mkutano na Waandishi wa Habari kwa lengo la kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya foleni iliyopo kwa sasa katika kituo cha kujaza gesi asilia kwenye magari cha Ubungo kutokana na hitilafu iliyotokea katika gari la kubeba gesi (CNG tanker) kupeleka kituo cha Anric TAZARA.
Dkt. Hudson amesema kuwa pamoja na kuharibika kwa lori hilo, foleni iliyopo katika kituo cha Ubungo kinadhihirisha mwitikio mkubwa wa wananchi wa matumizi ya gesi asilia kwenye magari.
Wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuweka mifumo ya gesi asilia kwenye magari kiasi kwamba vituo vilivyopo vinaonekana kuzidiwa na ili kutatua changamoto hii zipo jitihada mbalimbali ambazo TPDC inaendelea kuzifanyia kazi ambapo hadi sasa kampuni zipatazo 20 zimepewa leseni ya kujenga vituo vipya katika maeneo mbalimbali alieleza Dkt. Hudson.
Aidha katika adhma hiyo ya kuongeza vituo nchini, TPDC itajenga Kituo Kikuu (Mother station) katika maeneo ya Mlimani City chenye uwezo wa kuhudumia magari sita kwa wakati mmoja pamoja na malori sita ya kubeba CNG kwaajili ya kupeleka katika vituo vidogovidogo.‘’Nipende kuwahakikishia kwamba, uwepo wa kituo hiki kikubwa utasaidia kuongeza kasi ya uwepo wa vituo vingi vidogovidogo vya kujaza gesi asilia kwenye magari.‘’
Akiendelea kutoa ufafanuzi Dkt. Hudson amesema kabla ya mwisho wa mwaka huu vituo viwili vya kujaza gesi vinatarajiwa kujengwa na kampuni ya TAQA DALBIT katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na eneo la Sinza mkabala na Barabara ya Sam Nujoma ambapo vituo hivyo vitakuwa na karakana ya kuweka mfumo wa CNG.
Aidha, Dkt. Hudson amesema Kampuni ya TURKY Petroleum itajenga kituo eneo la Bagamoyo, Kampuni ya Anric itajenga eneo la Mkuranga, Kampuni ya BQ itajenga kituo eneo la Goba pia Kampuni ya DANGOTE itajenga eneo la Mkuranga. Uwepo wa Vituo hivi vyote vitasaidia kutatua changamoto za ujazaji wa gesi asilia kwenye magari.