Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii kwenye maeneo ambayo shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia zinafanyika. Huduma hizo ni pamoja na afya, elimu, maji na utawala bora ambapo huduma hizi ni sehemu ya Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR).
Hayo yamebainishwa katika ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC walipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na TPDC kupitia mpango wa uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii yaani ‘‘Corporate Social Responsibility’’ mkoani Mtwara.
Akitoa ufafanuzi wa miradi hiyo Meneja mradi Mhandisi Omari Kitiku alieleza kuwa, ‘’TPDC ilisaini hati ya makubaliano (MoU) ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Tsh. Bilioni 1.2 ambayo inatekelezwa katika Kata ya Msimbati na Madimba. Makubaliano hayo yalihusisha Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Kata ya Msimbati, Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Kata ya Msimbati pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya uwekaji wa taa za barabarani katika vijiji vya Msimbati, Mngoji na Madimba’’.
Aidha, Mhandisi Kitiku aliongeza kuwa ‘gharama za ujenzi wa miradi hiyo zinatofautina kulingana na aina ya mradi kama ‘Ujenzi wa kituo cha Afya unagharimu Tsh. Milioni 600 ambapo umefikia asilimia 80% ya ujenzi, Ujenzi wa kituo cha Polisi unagharimu Tsh. Milioni 186 na umefikia asilimia 65% pamoja na uwekaji wa taa za barabarani Tsh. Milioni 498 umefikia asilimia 15%.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bw. Ally Mluge alieleza namna TPDC inavyoshirikiana na jamii ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kuleta ustawi wa jamii na kuboresha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya TPDC na jamii zinazopitiwa na miundombinu ya gesi asilia.
‘‘Utekelezaji wa miradi hii ni sehemu ya jitihada za TPDC katika kukuza na kuboresha huduma na mahusiano na jamii zinazopitiwa na miundoimbinu ya gesi asilia,’’ alisema Mluge
Katika hatua nyingine Mhe. Rashidi Omary Linkoni, Diwani wa Kata ya Msimbati alishukuru uongozi wa TPDC kwa kuendelea na jitihada za kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo ambayo yanapitiwa na miundombinu ya gesi asilia. “TPDC kupitia jitihada zake za kusaidia jamii, inaongeza chachu ya kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo yetu, kwa hatua hii, naipongeza TPDC na tunaomba iendelee na jitihada hizi,” alisema Mhe. Linkoni.
- By:Beatrice Peter
- 0 comment