Wananchi wa Kinyagigi wafurahia Mradi  wa EACOP 


Wananchi wa Kata ya Kinyagigi Singida Vijijini waliopisha mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga wamesema,  wapo tayari kuchangamkia fursa mbalimbali kutokana na mradi huo.

Wananchi hao wa vijiji vya Kinyagigi na Mitula katika kata hiyo ambao kwa sasa wanahakikiwa maeneo yao na mali zao wamesema,  wanafurahi kupitiwa na mradi huo na wamejiandaa kuchangamkia fursa zitakazojitokeza.

Miongoni mwa wananchi hao wa Kinyagigi ni Bw. Ally Mtinangi ambaye amesema kuwa msimamizi wa mradi huo ambaye ni EACOP, mbali na  kulipa fidia amekuwa akitoa elimu ya ujasiriamali  na kilimo.

Mwenyekiti wa kijiji cha  Kinyagigi Musa Esya amesema,  hadi sasa hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

“Tunaendelea vizuri na hakuna lalamiko hata moja hadi sasa,  tupo vizuri na kuna waliokuwa wanashindwa kutafsiri lugha ya kiswahili lakini tumesaidia na kila mtu amepata haki zake. Tupo tayari kushirikiana na EACOP mwanzo hadi mwisho kujenga mradi utakaotunufaisha sisi na Watanzania wote,” ameongeza Esya.

Msimamizi wa fidia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Barnabas Yesaya amesema,  wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na zoezi linaendelea vizuri.

Katika kata ya Kinyagigi, kaya zilizopisha mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki  ni 59 kutoka kijiji cha Kinyagigi na 33 kijiji cha Mitula ambapo kwa  sasa zoezi linaloendelea ni kuhakiki taarifa zao.