Waziri Makamba Azindua Bodi Ya TPDC
Arusha, 4 Julai, 2022.
Mnamo tarehe 20 Mei 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alimteua Balozi Ombeni Sefue kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Kufuatia uteuzi huo mnamo tarehe 10 Juni 2022 Waziri wa Nishati, Mhe. January Y. Makamba (Mb) aliteua wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC ili kukamilisha safu ya bodi kwa mujibu wa sheria.
Kufuatia uteuzi huo, mnamo tarehe 4 Julai 2022 Waziri Makamba alizindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC kuashiria kuwakabidhi majukumu yao rasmi katika kuliongoza Shirika la TPDC. Akiongea wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Waziri Makamba alisema “TPDC ni miongoni mwa Mashirika ya Umma ya awali kabisa kuundwa baada ya kupata uhuru, hii ni kutokana na umuhimu wa Taifa kuwa na Shirika la Taifa la Mafuta na umuhimu wake umeendelea kuonekana hadi leo hii ambapo tuna ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia na shughuli za utafutaji wa mafuta zinaendelea sehemu mbalimbali katika nchi yetu”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue alisema “Tuna majukumu makubwa mbele yetu lakini niseme tu kuwa mimi ninaamini katika kufanya kazi kama timu yenye malengo ya pamoja na kwa utaratibu huo nina imani kuwa tutafika mbali na kutimiza ndoto za Rais wetu za kufunga magoli mengi (kupata mafanikio zaidi)”.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema “Siku ya leo ni kubwa na ya muhimu sana kwetu TPDC, tumekuwa tukijiendesha kwa kipindi cha miaka mitatu bila bodi baada ya bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake hivyo leo tunavyozindua bodi mpya tunajiskia faraja kama Taasisi”. Dkt. Mataragio alifafanua zaidi kwa kueleza kuwa TPDC imepata Bodi mahiri yenye watu wazoefu kwenye sekta ya mafuta na gesi na wabobezi katika uwekezaji na utendaji wa sekta binafsi.
- By:admin
- 0 comment