Zaidi Ya Asilimia 60 Ya Umeme unazalishwa na Gesi Asilia-Mwenyekiti Wa Bodi -PURA


Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Bwana Khalfan Khalfan leo tarehe 09/07/2022 ametembelea banda la TPDC katika Maonesho ya 46 ya Biashara jijini Dar es salaam na kutoa pongezi kwa TPDC kwa kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa katika uzalishaji wa umeme.

‘’Zaidi ya asilimia 60 ya umeme nchini unazalishwa na gesi asilia hivyo nawapongeza TPDC kwa kuhakikisha umeme unapatikana wa kutosha kwenye Gridi ya Taifa,’’ amesema Khalfan.

Akizungumza katika banda hilo, Bwana Khalfan amesema kiasi kikubwa cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini kina manufaa makubwa sana kwa Serikali na wananchi wake kwa ujumla.

Aidha, Khalfan ameyaomba Makampuni Binafsi na Wadau wa Sekta ya Nishati kuchangamkia fursa kwenye eneo la uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia ili kuongeza kasi ya usambazaji na wananchi wengi zaidi waweze kutumia rasilimali hiyo kwani Serikali peke yake haiwezi kuwafikia kwa muda mfupi.

‘’Mradi wa usambazaji wa gesi asilia kwa wananchi unahitaji fedha nyingi za ujenzi na uendeshaji wa miundombinu kwa sababu mwananchi anapounganishiwa gesi kwa ajili ya matumizi ile ni huduma na sio biashara’’.

Vilevile amewasisitiza wananchi kutumia gesi asilia kwenye magari ili waweze kupunguza gharama za maisha.

Serikali kupitia TPDC mpaka sasa imeunganisha nyumba 1,500 na mtandao wa gesi asilia kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es salaam, zaidi ya magari 1,500 yanatuma gesi asilia pamoja na viwanda 48 kwa mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Mtwara.