Gesi Asilia Kukuza Sekta ya Viwanda

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea na zoezi la kutoa elimu
kwa wananchi mbalimbali waliohudhuria kwenye Maonesho ya Saba ya Viwanda yenye
kauli mbiu ‘’Nunua Bidhaa za Tanzania Jenga Tanzania’’ yanafanyika katika viwanja
vya Mwl. J.K Nyerere jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika Maonesho hayo Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
Bi. Marie Msellemu amesema lengo la TPDC ni kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi
asilia kwenye viwanda, magari na majumbani ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi
na kuitumia nishati hiyo.
Bi. Msellemu amesema mpaka sasa zaidi ya Viwanda 53, magari 1500 na nyumba
1520 zimeshaunganishwa na mtandao wa gesi asilia katika Mikoa ya Mtwara, Lindi,
Pwani na Dar es salaam.’’TPDC ni mdau mkubwa katika Sekta ya viwanda na ndio
maana tumeshiriki katika maonyesho hayo ili kubaini changamoto mbalimbali kutoka
kwa wadau wa viwanda ili zitusaidie kuboresha huduma zetu pia kupokea pongezi kwa
maeneo yanayofanya vizuri.’’
Aidha, Bi. Msellemu amesema gesi asilia ina mchango mkubwa katika kuzalisha
umeme nchini ambapo mpaka sasa zaidi ya asilimia 60 ya gesi asilia inatumika
kuzalisha umeme.
Halikadhalika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Dkt. Jim Yonazi amewapongeza TPDC kwa kuanzisha mfumo wa gesi asilia wenye
gharama nafuu kwa wananchi. Pia amewaomba kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi ya
usambazaji gesi asilia kwa Mikoa yote Nchini.