Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefurahishwa na matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika Sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.

Hayo yamejiri wakati wa ziara maalumu ya Kamati hiyo ilipotembelea mitambo ya uchakataji gesi asilia ya Mnazi bay na Madimba Mkoani Mtwara.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deus Sangu (Mb) alisema kuwa Kamati imefurahishwa na matokeo ya uwekezaji uliofanywa na unaoendelea kufaywa na Serikali katika Sekta ya Mafuta na gesi asilia hapa nchini.

“Kazi kubwa imefanyika tangu Shirika hili la TPDC lilipoanzishwa mwaka 1969 ambapo uthubutu wa Serikali kuwekeza katika sekta hii umeleta matokeo chanya kama haya ya TPDC kununua asilimia 20 ya hisa za Kampuni ya Wentworth Resources na kupelekea TPDC kufikia asilimia 40 ya hisa sawa na bilioni 106.4 za kitanzania katika Kitalu cha Mnazibay na hivyo kuipa nguvu Kampuni hiyo ya umma katika maamuzi ya uendeshaji wa Kitalu”, alisema Mhe. Sangu.

Aidha Mwenyekiti wa Kamati alibainisha kuwa matokeo mengina chanya ya uwekezaji katika sekta ya gesi asilia ni pamoja na kulihakikishia taifa uwepo wa nishati ya umeme ambapo zaidi ya asilimia 65 ya umeme katika gridi ya Taifa unazalishwa kupitia gesi asilia.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Vuma Augustino (Mb) alipongeza uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mafunzo kwa vijana wa kitanzania nje ya nchi ili kuweza kufanya uendeshaji wa shughuli za uzalishaji wa gesi asilia.

“Kwa niaba ya Kamati yetu na Wajumbe wenzangu, naipongeza sana Serikali, tumefurahishwa na namna ambavyo nafasi zote katika kiwanda zimeshikwa na vijana wa Kitanzania ambapo huko nyuma Serikali ilikuwa ikilipa mabilioni ya fedha kwa waendeshaji kutoka nje ya nchi”, amebainisha Mhe. Vuma.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Mhe. Balozi (mstaafu) Ombeni Sefue, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamati ya PIC na Wabunge wote kwa ujumla kwa miongozo thabiti katika kusimamia rasilimali hii na kuahidi kuhakikisha kuwa rasilimali ya gesi asilia inatumika katika kuleta maendeleo ya nchi na katika maeneo ambayo rasilimali inapatikana.

Kamati ya PIC imehitimisha ziara yake kwa miradi ya gesi asilia baada ya kufanya katika Mkoa wa Mtwara ikiwa ni jukumu lake la kiutendaji la kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali kupitia taasisi zake mbalimbali unatekelezwa kwa kuzingatia tija kwa Taifa.