Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya uzinduzi rasmi wa Kiwanda cha uwekaji mifumo mbalimbali katika mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta ghafi mradi wa EACOP kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania tarehe 26.03.2024.

Dkt. Biteko amesema kwamba ujenzi wa Mradi huo unaendelea vizuri ambapo hadi sasa kwa upande wa eneo la kuhifadhia mafuta ujenzi wa matenki makubwa manne Chongoleani Tanga umefikia asilimia 37 huku ujenzi wa gati kwaajili ya kupakia mafuta ukiwa umefikia asilimia 36.  Tayari vipande elfu 16 vya mabomba yenye uwezo wa kutandaza urefu wa kilomita 300 za bomba zimekwisha wasili katika eneo la Sojo, Nzega Mkoani Tabora.

Aidha Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wazawa katika fursa mbalimbali za ajira zinazozalishwa na mradi.  “Serikali haitaruhusu fursa za kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania ziende kwa wasio Watanzania,” amesema Biteko.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Mandeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, amesema kuwa Tanzania na Uganda zinaendelea kushirikiana kusimamia mradi wa Bomba la Afrika Mashariki (EACOP) ili kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga, Tanzania kwa maslahi ya Wananchi wa mataifa hayo na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Dkt. Nankabirwa amesema, kati ya visima 426 tayari visima 26 vimechimbwa nchini Uganda na kasi ya uchimbaji inaendelea vizuri ili kupata mafuta ya kutosha.

“Nawaomba wadau na washirika wote wa mradi huu waendelee kushirikiana na kuweka nguvu kufikia malengo. EACOP wamepokea vibali kutoka Uganda na Tanzania, hivyo tumefika hatua ambayo hatuwezi kurudi nyuma,” amesisitiza Dkt. Nankabirwa.