Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzani (TPDC) na Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Msumbiji (Empresa Nacional de Hidrocarbonetos-ENH) zimekubaliana kuanzisha ushirikiano wa kimkamkati katika sekta ya utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za gesi asilia na mafuta.

Makampuni hayo mawili yamekutana Jijini Dar es salaam kwa ajili ya majadiliano ya kushirikiana ambapo TPDC ilitoa mualiko kwa ENH kwa lengo la kuanzisha majadiliano hayo muhimu kwa nchi zote mbili.

Akiongea baada ya kikao kazi kilichofanyika Februari 7, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema “Tanzania na Msumbiji tayari tuna mahusiano ya kindugu toka wakati wa harakati za ukombozi wa bara la Afrika, tunataka kuendeleza mahusiano yetu katika sekta ya mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya nchi zetu mbili.”

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa ENH, Dkt. Estevão Pale alieleza namna ambavyo wanaona Tanzania imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika kipindi cha muda mfupi jambo ambalo linaashiria uongozi wenye dira na mipango thabiti, “nimeona tofauti kubwa ya kimaendeleo leo hii nikilinganisha na miaka 10 iliyopita ambayo nilikuja Tanzania”. Dkt. Pale alifafanua kuwa moja ya vitu vinavyomvutia Tanzania ni namna ambavyo nchi imeweza kutumia gesi asilia kuzalisha umeme jambo ambalo limeisaidia nchi kuepukana na upungufu wa umeme hususan kipindi cha kiangazi.

ENH wametembelea Tanzania kwa mualiko kutoka TPDC kwa lengo la kuanzisha mazungumzo ambayo yatawezesha kampuni hizi mbili kushirikiana katika nyanja mbalimbali kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia.

Msumbiji ina hifadhi kubwa ya gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 100 na wanatekeleza miradi kadhaa ya kuzalisha gesi asilia ikiwemo miradi ya LNG.