Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Zambia, Mhandisi Himba Cheelo amefanya ziara ya kutembelea mitambo ya kupokea gesi asilia  inayosimamiwa na GASCO Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) iliyopo Kinyerezi Jijini Dar es Salaam.

Akiwa katika mitambo hiyo Mhandisi Cheelo amesema,  lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna Tanzania imepiga hatua katika suala la uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali.

“Zambia imefanya mabadiliko makubwa katika suala zima la uagizaji na uingizaji wa mafuta ya petroli ambapo kufikia Septemba 30, 2022 Serikali ya Zambia ilijiondoa rasmi katika jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na kuachia jukumu hilo kwa sekta binafsi,” amesema Cheelo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Tanzania, Heri Mahimbali amesema wamefurahi kupokea ugeni huo na wapo tayari kuwapatia wanachokihitaji.