EACOP Mambo Safi


Manyara,

Wakazi wa Kijiji cha Njoro Kata ya Kibaya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wameishukuru Serikali kwa kuendeleza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP),  kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga.

Wakizungumza na Mwandishi wa  Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakazi hao wamesema,  wako tayari kuchangamkia fursa za ujenzi katika mradi huo. 

Mwalimu Clemenciana Shayo ni miongoani mwa watu  waliopisha mradi huo na kulipwa fidia ambaye  amesema kuwa,  ameridhika nayo na anafurahi mradi huo kupita kijijini kwao kwani  utafungua fursa mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,  Mhe. Mbaraka Batenga amesema,  elimu imeshatolewa kwa wananchi juu ya fursa zinazopatikana katika mradi huo wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo  imeendelea kijiimarisha katika ulinzi wa bomba hilo kuanzia hatua za awali na utakapoendelea. 

Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki  kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani,  Tanga lina  urefu wa  kilomita 1,447 na hadi kukamilika kwake ujenzi wake unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi  trilioni 11.